Majaliwa kupokea watalii 343 wanaotua Tanzania leo

Muktasari:

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo jioni Jumapili Mei 12 atawapokea watalii 343 kutoka China wakiwamo wafanyabiashara na watu maarufu, wawekezaji kutoka kampuni 27, waandishi wa habari 40, maofisa wa Serikali ya China na mawakala wa kampuni za utalii wanaokuja  kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii kwa siku tano.

Arusha.  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo jioni Jumapili Mei 12  anatarajiwa kuwapokea watalii 343 kutoka China wanaokuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii kwa siku tano.

Mara baada ya watalii hao kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) itafanyika hafla fupi ya kuwakaribisha na kesho wataanza safari ya kutembelea vivutio  huku baadhi yao wakishiriki kongamano la uwekezaji sekta ya utalii litakalofanyika kesho.

Ujio wa watalii hao unatokana  Bodi ya Utalii (TTB) kuingia makubaliano na kampuni ya Touchroad International Holdings Groups ya China Novemba mwaka jana wakati wa ziara ya kutangaza utalii katika miji ya Beijing, Shanghai, Chengdu, Guangzhou na Hong Kongna nchini China.

Wanaowasili leo ni wafanyabiashara na watu maarufu, wawekezaji kutoka kampuni 27, waandishi wa habari 40,

maofisa wa Serikali ya China na mawakala wa kampuni za utalii.

Akizungumza na Mwananchi,  mtendaji wa TTB, Devotha Mdachi amesema:  “ Wageni hawa watapokelewa pia na Waziri wa Maliasili na Utalii,  Dk Hamisi Kigwangala, katibu mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda na mwenyekiti wa TTB, Jaji mstaafu Thomas Mihayo.”

Watalii hao watatembelea Hifadhi ya Taifa ya Manyara, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Olduvai Gorge, Maboma ya Wamaasai, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na baadaye wataelekea  vivutio vya utalii vya Zanzibar.

Meneja mahusiano wa TTB, Geofrey Tengeneza amesema maandalizi yote ya ujio wa watalii hao yamekamilika.

"Dhamira ya TTB kutangaza utalii katika soko la China na Juni mwaka huu wanatarajia kufanya ziara ya kutangaza utalii katika miji ya Nanjing,  Hanzhou na Changsha,” amesema.