Majambazi wajifanya matrafiki, watapeli madereva magari ya IT

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Musilimu 

Muktasari:

Baadhi ya madereva wanaoendesha magari yanayokwenda nchi mbalimbali kupitia Tanzania (IT) wameibua madai ya watu wanaojifanya askari wa usalama barabara na kuwadai fedha


Dar es Salaam. Baadhi ya madereva wanaoendesha magari yanayokwenda nchi mbalimbali kupitia Tanzania (IT) wameibua madai ya watu wanaojifanya askari wa usalama barabara na kuwadai fedha.

Takribani wiki mbili zilizopita madereva hao wamedai wenzao watano wamekumbana na matrafiki hao feki maeneo ya Kimara na Mbezi jijini Dar es Salaam wakati akitokea Bandari ya Dar es Salaam kupeleka magari katika nchi hizo.

Alipoulizwa na Mwananchi juzi Ijumaa Julai 12, 2019 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema hawajapata taarifa za uwepo wa matukio hayo, kuahidi kufuatilia.

Kwa mujibu wa maelezo ya madereva hao, askari hao feki hutumia foleni katika maeneo hayo kuwasimamisha na kuibua makosa mbalimbali na kudai fedha ili kuwaachia.

“Wametengeneza vitambulisho kujitambulisha kama maofisa wa polisi na huvaa nguo za kiraia. Mara nyingi huwatajia madereva kosa la kutosimama kwenye alama za kuvuka watembea kwa miguu,” amesema Dumisani Mpofu.

Mpofu amesema aliporwa na watu hao Dola 300 za Marekani na fedha ya Tanzania.

Amesema watu wanne walifika kwenye gari lake akiwa katika foleni eneo la Kimara, kutoa kitambulisho wakidai ni askari na kumtaka ashuke kwenye gari.

“Niliteremka kwenye gari kama walivyoagiza kwa kuwa walitoa kitambulisho, sikuwatilia shaka kwa kuwa ilikuwa saa mbili usiku.”

“Baada ya foleni kuanza kutembea walinitaka nipeleke gari kituo cha polisi kupitia kwenye barabara ya pembeni. Nilijaribu kujitetea kuwa sijafanya kosa lolote lakini hawakunisikiliza, nakumbuka walisema natakiwa kulipa faini ya Sh250,000,” amesema.

Ameongeza, “Tulisimama kwenye kilima kidogo kulikuwa na giza na hapo ni baada ya kila mbinu kushindikana. Watu watatu waliokuwa wamekaa siti cha nyuma walinitaka kutoa fedha zote nilizokuwa nazo.”

Amesema aliwapatia kiasi hicho cha fedha na baadhi walianza kumpekua, “Niliondoa gari na kumgonga wa mbele, waliokuwepo ndani wakashuka na nilifanikiwa kuondoka eneo hilo.”

“Baada ya kurudi barabara kuu niliendesha umbali mrefu bila kukutana na polisi walionionyesha vitambulisho. Nikaona nimeshatapeliwa.”

Kabla ya Mwananchi kuzungumza na Mpofu, katika mitandao ya kijamii zilisambaa taarifa za dereva huyo kutapeliwa na askari hao feki.

Katika ufafanuzi wake, Mambosasa amewataka wanaofanyiwa vitendo hivyo kutoa taarifa polisi.

“Hatuna hizo taarifa nadhani kama kuna dereva amepatwa na mkasa huyo sehemu sahihi ya kwenda ni kutoa taarifa kituo cha polisi kilichopo karibu,” amesema Mambosasa.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Musilimu amesema kuna matukio ya uhalifu yasiyohusiana na kitengo cha trafiki.

“Sina hizo taarifa lakini hayo ni makosa ya jinai siyo ya trafiki. Hayo matukio hayajaripotiwa kwetu japo watu wanaoyatekeleza wanajifananisha na trafiki lakini kwa kweli siyo makosa ya trafiki,” amesema Muslimu.