Majeruhi mwingine ajali ya Morogoro afariki, vifo vyafikia 76

Tuesday August 13 2019

 

By Lilian Lucas, Mwananchi

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro  (RC) nchini Tanzania, Dk Stephen Kebwe amesema vifo vinavyotokana na ajali ya mlipuko wa moto iliyotokea Jumamosi iliyopita ya Agosti 10, 2019 mkoani humo vimeongezeka na kufikia 76.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Agosti 13,2019 nje ya chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, RC Kebwe amesema idadi hiyo imefikia baada ya majeruhi mmoja aliyelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kufariki usiku wa kuamkia leo.

Amesema majeruhi waliosafirishwa kwenda Muhimbili wengi walikuwa katika hali mbaya kwa sehemu kubwa ambapo mpaka sasa (asubuhi) wamebakia 38 wakiendelea na matibabu na katika Hospitali ya Rufaa Morogoro wamebaki 16 nao wakiendelea na matibabu.

Mkuu huyo wa mkoa amesema miili iliyobaki mpaka leo asubuhi ni nane na kati ya hiyo sita imetambuliwa na ndugu na taratibu za mazishi zinaendelea ambapo mchana wa leo kuna mmoja atazikwa katika makaburi ya Kola Morogoro na miili miwili haijatambuliwa.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema kila kifo kinachotokea kinahifadhiwa sehemu husika na kuchukua vipimo vya vinasaba (DNA) ili ndugu akipatikana aweze kumtambua ndugu zao.

Amesema kuanzia leo Jumanne, timu ya maafa ya kitaifa itakabidhiwa kwa timu ya maafa ya mkoa na kuendelea na taratibu zingine.

Advertisement

Advertisement