Makamba: Ruge alinishauri nigombee urais mwaka 2015

Muktasari:

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema mkurugenzi wa vipindi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba ndiye alikuwa wa kwanza kumtaka achukue fomu za kuwania urais mwaka 2015


Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema mkurugenzi wa vipindi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba ndiye alikuwa wa kwanza kumtaka achukue fomu za kuwania urais mwaka 2015.

Makamba ameeleza hayo leo Jumanne Februari 19, 2019 katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, ikiwa ni siku moja baada ya familia ya Ruge kuomba msaada kwa Watanzania kumchangia fedha ndugu yao anayetibiwa nchini Afrika Kusini.

“Mtu wa kwanza kuweka kichwani mwangu wazo la kuchukua fomu kubwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 alikuwa Ruge,” amesema Makamba.

“Alifanya hivyo mwaka 2010, miaka mitano kabla, wakati email (barua pepe) hii aliyoniandikia akiwa safarini Marekani. Na alitoa sababu zake nzito.”

Makamba aliweka sehemu ya barua ya Ruge aliyomuandikia akimshauri kuwania urais, “Nimefikiria sana muda wote njiani wakati natokea TZ (Tanzania)..., nadhani ugombee urais mwaka 2015.”

Katika mchakato wa kura ya maoni ndani ya CCM mwaka 2015, Makamba aliingia tano bora pamoja na Bernard Membe, Dk Asha Rose Migiro, Balozi Amina Salum Ali na Rais John Magufuli.

Rais Magufuli alishinda kwa kupata asilimia 87 ya kura zote za wajumbe, huku wengine walioingia tatu bora; Balozi Amina alipata asilimia 10 na Dk Asha Rose Migiro asilimia tatu.