Makamba atoa kauli ya kwanza, Zitto amkaribisha

Muktasari:

  • Aliyekuwa waziri wa ofisi ya makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba ametoa kauli yake ya kwanza baada ya kutenguliwa katika nafasi hiyo huku mbunge mwenzake wa Zitto Kabwe akimkaribisha kuendelea na kazi za kibunge

Dar es Salaam. Baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa waziri ofisi ya makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba na nafasi yake kumteua mwingine, Makamba ametoa kauli yake ya kwanza baada ya uamuzi huo.

Taarifa ya Ikulu iliyotoka leo Jumapili na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Julai 21, 2019 imeeleza Rais Magufuli amemteua George Simbachawene kuchukua nafsi ya Makamba aliyedumu katika nafasi hiyo tangu Desemba mwaka 2015.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter Makamba ameeleza kupokea taarifa hiyo na kuahidi kutoa kauli yake siku zijazo

“Kwa kweli nimeyapokea mabadiliko yaliyofanywa kwa moyo mweupe kabisa kabisa

. Nitasema zaidi siku zijazo,” ameandika Makamba ambaye ni Mbunge wa Bumbuli (CCM) huku akiambatanisha na picha yake akiwa na Rais mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi wakiwa wanatabasamu

Katika hatua nyingine Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe ametumia ukurasa wake wa Instagram kumkaribisha mbunge mwenzake Makamba kukaribia tena ‘Backbench’ (nafasi za nyuma ndani bungeni) kuendelea na kazi ya Ubunge

Zitto katika ukurasa wake wa Instagram anaotumia jina la zittokabwe ameeleza baadhi ya sifa za mbunge huyo wa Bumbuli huku akiambatanisha na picha waliyokuwa pamoja nje ya Bunge la Tanzania.

“Rafiki yangu @HYPERLINK "https://www.instagram.com/jmakamba/"jmakamba karibu tena Backbench tuendelee na kazi. Ulikuwa Mbunge bora sana back bench 2010-2012 na ninaamini itakuwa hivyo tena 2019-2020.”

“Umekuwa mmoja wa mawaziri bora kabisa ambao umeonyesha tofauti ya kutawala na kuongoza. Namna ulivyoongoza marufuku ya mifuko ya plastiki ilionyesha falsafa yako ya uongozi ni tofauti sana na falsafa ya Serikali yenu ya CCM.”

Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo ameendelea kusema, “Tuna kesho nyingi tupambane kuijenga Tanzania inayojali watu wake na ya kidemokrasia.”