Makonda abaini upigaji vitambulisho vya machinga Kariakoo

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda  wa pili kutoka kulia akizungumza na mchuuzi wa matunda, Edward Mesco alipofanya ziara eneo la Kariakoo ya kukagua wafanyabiashara wenye vitambulisho.

Muktasari:

  • Makonda awatembelea wamachinga wa Kariakoo abaini baadhi yao kutumia vitambulisho vya kufoji, kukodishana  na kuazimana.
  • Waliobanika wachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kushikiliwa na vyombo vya dola na kuwaonya wengine wenye tabia hiyo.


Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amebaini mambo matatu kwa wafanyabiashara wadogo eneo la Kariakoo kuhusu matumizi ya vitambulisho vya biashara vilivyotolewa na Rais John Magufuli.

Mambo hayo ni vitambulisho viliyotolewa na Serikali vimeanza kughushiwa, wamachinga kuazima vitambulisho huku wengine wakikodishana wenyewe kwa wenyewe kwa Sh1,000 ili ukaguzi unapofanyika mfanyabiashara aonekane yupo salama.

Makonda ameeleza hayo  leo, Jumanne Juni 4, 2019 wakati wa ziara ya kukagua wamachinga wenye vitambulisho na wasiokuwa navyo katika mitaa mbalimbali ya Kariakoo ikiwemo ya Msimbazi na Kongo, akiambatana na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

“Ni kosa la kisheria kufoji nyaraka za Serikali , nimeshawaelekeza na hatua kali zimeshachukuliwa  kwa wale wote waliobainika kuwa na vitambulisho ‘fake’.”

“Masikitiko yangu baadhi ya wamachinga wameamua kutokuwa waaminifu, badala ya kulipa kitambulisho kwa Sh20,000 ili apate chake wameamua kutoa ‘photocopy’ amesema Makonda kwenye ziara hiyo.

Kwa mujibu wa Makonda, takwimu ndogo alioifanya katika watu 10, wanne hawana kabisa vitambulisho hata vile vichache ambavyo maofisa wake walivibeba kwenda kwa ajili ya kuwapa wamachinga wasiokuwa navyo vimeisha kabla ya kumaliza ziara yake.

“Tafsiri yake ni kwamba watu wengi walioko  Dar es Salaam, hawana vitambulisho. Ndugu za wamachinga hakuna sababu ya kufoji na kukodi hakikisha unatii sheria bila shuruti, ukifanya biashara kwa kitambulisho chake utaheshimika,” amesema Makonda.

Katika ziara hiyo, baadhi ya wafanyabiashara akiwemo Allen Yohana ambaye hakuwa na kitambulisho alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuelezwa na Makonda achague jambo moja kufunga biashara yake au afanye usajili wa kupata kitambulisho kwa maofisa walioambatana na Makonda.

Baada ya kujifikiria kwa dakika kadhaa, Yohana aliamua kuandikisha jina kwa ajili ya kupata kitambulisho hicho, ili kuepuka kufunga biashara yake.