Makonda atangaza neema kwa wafanyakazi Dar

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amemuagiza katibu tawala wa mkoa (Ras) na wakurugenzi wa manispaa kuhakikisha kila mfanyakazi anayestahili kupanda daraja apandishwe kabla Mei haijaisha

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amemuagiza katibu tawala wa mkoa (Ras) na wakurugenzi wa manispaa kuhakikisha kila mfanyakazi anayestahili kupanda daraja apandishwe kabla mwezi Mei haujaisha.

Makonda ameyasema hayo leo Mei Mosi kwenye sherehe ya maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani kimkoa ambayo yamefanyika katika uwanja wa Uhuru.

Amewataka maofisa utumishi wabadilike vinginevyo watabadilishwa wao. Amesema watumishi hao wamekuwa hawatoi likizo kwa watumishi wanaostahili, jambo ambalo linatengeneza matabaka sehemu za kazi.

 

"Wenye sifa ndani ya mwezi huu lazima wawe wamepandishwa madaraja. Kwa hiyo, Ras na timu yako mjipange kutimiza takwa hili la kisheria," amesema Makonda na kushangiliwa na watumishi waliohudhuria sherehe hizo.

Awali akizungumza kwenye sherehe hizo, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) mkoa wa Dar es Salaam, George Faustine alisema changamoto kubwa inayowakabili wafanyakazi ni kutopandishwa madaraja licha ya kwamba wana sifa zote.

Faustine amebainisha pia kwamba wafanyakazi wengi wanafanya kazi nyingi zisizokuwa zao, jambo ambalo linapunguza morali na ufanisi sehemu za kazi.

Baadhi ya wafanyakazi waliohudhuria sherehe hizo wameitaka Serikali kuongeza mishahara na kupandishwa madaraja kwa sababu gharama za maisha zimepanda.

"Tunachohitaji ni nyongeza ya mishahara na kupandishwa madaraja. Hicho ndiyo kilio chetu tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani," amesema mwalimu mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Naye mwanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Simon Mwangosi amemshukuru mkuu huyo wa mkoa kwa kuagiza watumishi kupandishwa madaraja lakini ameomba upandaji wa madaraja uende sambamba na ongezeko la mishahara.