Manispaa Ilala yanyang’anywa Sh3 bilioni

Tuesday February 19 2019

Naibu waziri wa fedha na Mipango, Dk Ashatu

Naibu waziri wa fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali imeinyang'anya Manispaa ya Ilala, mkoani Dar es Salaam Sh3 bilioni ilizoipatia kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kimkakati wa machinjio ya kisasa ya Vingunguti.

Uamuzi huo umetokana na manispaa hiyo kushindwa kutekeleza kwa wakati mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh8.5bilioni.

Hayo yameelezwa na naibu waziri wa fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo.

Amesema Serikali ilitoa Sh3 bilioni kati ya Sh8.5 bilioni  kukamilisha mradi wa machinjio ya Vingunguti kuanzia Mei, 2018, lakini hadi sasa  fedha hizo hazijatumika.

“Fedha haziwezi kukaa kwa mwaka mzima bila matumizi ilihali kuna maeneo mengine ambako fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi, hivyo tunazichukua fedha hizi na Manispaa ya Ilala mtalazimika kuomba upya mtakapokuwa mmejipanga," alieleza Dk Kijaji.

Alibainisha kuwa kwa mujibu wa taratibu za fedha za Serikali zinazopelekwa kwenye miradi zinatakiwa zianze kutumika ndani ya miezi mitatu lakini Manispaa ya Ilala haijazitumia fedha hizo huku karibu Mwaka wa Fedha ukikaribia kumalizika.

"Tunaiangusha dhamira njema ya Mheshimiwa Rais Dk John Pombe Magufuli ya kuwahudumia Watanzania waliosubiri kuhudumiwa, ndio maana tukaanzisha miradi hii ya kimkakati ya kuongeza mapato ya halmashauri na mkaleta maandiko yenu Serikali ikatoa fedha kumbe hamko tayari na mnatukwamisha kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi," alisema.

"Tumewapatia fedha mmeshindwa, kwa hiyo wana Ilala na wana Vingunguti, kwamba Serikali yao ina dhamira njema lakini wapo wanaotuangusha hivyo tutazichukua fedha hizi mpaka hapo Manispaa ya Ilala watakapoleta mpango kazi unaotekelezeka na si huu ambao hawakujiandaa," alisisitiza.

Dk Kijaji alisema kuwa kabla ya kuomba fedha za miradi ya kimkakati ni lazima masuala yote ya upembuzi yakinifu yawe yamefanyika na kama hayakufanyika basi manispaa ilimdanganya katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na waziri mwenyewe ambaye aliridhia Ilala ipewe fedha hizo.

Naye naibu kamishna wa bajeti wa wizara ya Fedha, Dk  Charles Mwamwaja, alisema kuwa manispaa ya Ilala, imekiuka mkataba ama makubaliano ya kupewa ruzuku ya Sh8.5 bilioni kwa ajili ya mradi huo na ni lazima sheria ya fedha ichukue mkondo wake kwa kuzirejesha fedha hizo Mfuko Mkuu wa Hazina hadi watakapo kuwa tayari.

Kwa upande wake ofisa mipango wa manispaa ya Ilala, Ando Mwankuga, alikiri kuwa kulikuwa na ucheleweshaji wa kuanza kutekeleza mradi huo kwa kile alichodai ni kuchelewa kwa mchakato wa kufanya ununuzi na mabadiliko ya mara kwa mara ya kiufundi kutoka kwa mtaalam mshauri wa mradi huo.

"Ucheleweshaji huu si wa makusudi bali ilikuwa ni kuhakikisha tunafuata taratibu zote za ununuzi na kuhakikisha mradi utakaojengwa uwe na ubora unaotakiwa na unaolingana na thamani ya fedha na tunatarajia kuanza kuutekeleza Machi 10, 2019" aliongeza.

Manisapaa ya Ilala, ilikuwa miongoni mwa halmashauri na manispaa 17 nchini zilizopatiwa ruzuku na Serikali kiasi cha zaidi ya shilingi 147 bilioni katika awamu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati itakayochochea upatikanaji wa mapato ya ndani na kuzijengea uwezo Serikali za mitaa na miradi hiyo inatakiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 18 kuanzia Mei, 2018.

Advertisement