MAHUBIRI YA JUMAPILI: Maono ya kiungu au nguvu ya maono

Muktasari:

  • Naitwa Askofu Jacob Chimbwegu wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (KLPT), parishi ya Geza Ulole- Kigamboni

Leo nitazungumzia kuhusu maono. Maono ni picha ya tukio au kitu Fulani kinachoonekana kwa dhahiri wakati mtu akiwa na ufahamu wake wa kawaida. Mungu huonyesha picha halisi au tukio fulani na hutokea katika hali isiyokuwa ya kawaida ili kufundisha juu ya jambo fulani.

Maono yasichanganywe na ndoto, mawazo au mafunuo. Mambo haya kwa ujumla wake hubeba maana tofauti na namna ya utokeaji wake huwa tofauti.

Mathayo 17:9: “Walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu akawaambia: ‘Msimwambie mtu yeyote maono haya mpaka mimi Mwana wa Adamu nitakapofufuliwa kutoka kwa wafu.”

Matendo 7:31: “Musa alipouona, akastaajabia maono yale, na alipokaribia ili atazame, sauti ya Bwana ikamjia.”

Mara nyingi watu wengi wamekuwa wakishindwa kutofautisha na hivyo kuishia kusema nimepata ufunuo kumbe ni maono au ni ndoto.Somo hili limelenga kutupa ufahamu wa kutofautisha mambo haya ili tupate uelwa wa namna Mungu ananyotusemesha .

Mafunuo

Mafunuo ni mawasiliano kati ya ufahamu wa Mungu na nafsi ya mwanadamu.

Mathayo11:25: “Wakati huo Yesu alisema: ‘Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima na wenye elimu mambo haya, ukawafunulia wadogo. 26 Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza.”

Kwa lugha rahisi mafunuo ni ufahamu wa mawazo ya Mungu kupitia akili ya mwanadamu. Hivyo, kwa ujumla ufunuo unaiwezesha akili ya mwanadamu kufahamu kwa undani mambo yaliyoko katika moyo wa Mungu au hekima ya kiungu.

Mungu huruhusu hili kwa kusudi maalumu na wakati maalumu kwa wanadamu waliojiandaa kuwa tayari kupitishia mambo ya kiungo kwao. Si kila mtu anaweza kutumiwa, ingawa hakuna mtu maalumu kwa ajili ya kupokea mafunuo.

Wafilip 3:15: “Sisi tuliokomaa kiroho tuwe na msimamo kama huu. Lakini kama kuna mawazo tofauti kuhusu jambo lolote, Mungu atawafunulia.”

Yohan 12:8, mthayo 16:17

Ndoto ni mawasiliano ya Mungu na ufahamu wa mwanandamu kuonyesha picha ya tukio au jambo wakati mwanadamu akiwa amelala. Mungu alitumia njia kuongea na watu wa kale katika Biblia na huitumia hata sasa.

Ndoto zinaweza kusababishwa na matukio kadhaa yakiwamo shughuli za kila siku na kujirudia unapolala kama picha ya kilichotoea, ndoto huweza tokana na kuugua ama kisaikolojia au ndoto hutokana na Mungu, lakini zinatokana na adui shetani kuonyesha matukio fulani hupitia ufahamu wa mwanadamu.

Mwanzo 37:5-11: “Baada ya muda Yosefu aliota ndoto, akawasimulia ndugu zake, nao wakawa na sababu zaidi ya kumchukia. 6. Aliwaambia hivi: “Tafadhali, sikilizeni ndoto hii ambayo nimeota. 7. Tazama, tulikuwa tukifunga miganda katikati ya shamba wakati ambako mganda wangu uliinuka, ukasimama wima nayo miganda yenu ikauzunguka na kuuinamia mganda wangu. 8 Nao ndugu zake wakamwambia: ‘Je, kwa kweli utakuwa mfalme juu yetu? Au utatutawala?”

Shetani hupenda kutumia njia hii kuingiza fikra potofu katika ufahamu wa mwanadamu ili kumhamisha katika imani yake.

Hivyo, ndoto zinaweza kuwa wazi lakini ndoto nyingine zimefungwa hivyo zinahitaji tafsiri ili kupata maana/taarifa sahihi inyoelezewa katika ndoto hiyo.

Hapa ndipo hekima ya Mungu inahitajika inyoweza kukuhekimisha kujua hii imetoka kwa Mungu na tafsri yake ni ipi, au imetokana na adui shetani au shughuli na uchovu wa kazi za siku.

SEHEMU YA KWANZA

Nini hutokea kama hakuna maono.

Mithali 29:18: “Pasipo maono, watu huacha kujizuia; bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.”

Maono yanamjenga mwanadamu katika kuweka misingi na wigo wa namna gani aishi huku akimpendeza Mungu. Yaani nini afanye au asifanye kwa wakati gani na mahali gani ili Mungu afurahi.

Pasipo maono hakuna kujizuia hivyo lazima kumkosea Mungu na hatimaye kujikuta dhambini. Mshahara wa dhambi ni mauti (yaani jehanamu ya moto).

Maono huumba picha na mipaka ya kuifikiria picha hiyo. Mungu anataka kutuwekea picha ile iliyomo ndani yake ili nasi tuwe nayo kisha tuufurahie wema wake.Neno la Mungu linatukumbusha: “Nayajua mawazo ninayo wawazia ninyi asema bwana, mawazo ya kuwastawisha…” hii ndio picha Mungu anataka tuwe nayo.

Bila maono hakuna namna ya kujidhibiti hivyo mwanadamu anaenda kama anavyoona ni sawa machoni pake mwenyewe. Tutasahau wema wa Mungu, tutasahau maagizo yake na madahara ya kutoyatekeleza na mwisho hakutakuwa na nidhamu ya kimungu ndani ya mtu. Mwisho huwa ni uangamivu na kupotea katika ramani ya Mungu. Watu wengi wameacha imani ya wokovu kwa kuona Ukristo ni shida, ni mgumu na adui amewapiga ganzi wasione Mungu anavyotaka wawe ili waangamie kwa kukata tamaa, kulaumu kila kitu na kutochukua hatua za imani kutatua tatizo.

Anapatikana kwa namba 0714776443