Masharti mapya mikopo ya ardhi

Dar es Salaam. Mtu binafsi au kampuni inayotaka kutumia hati ya kumiliki ardhi kama dhamana ya mkopo wa kuendeleza ardhi kutoka benki za nje au ndani ya nchi atalazimika kutoa tamko kuwa fedha hizo zitawekezwa Tanzania, kwa mujibu wa kanuni mpya za matumizi ya ardhi.

Kanuni hizo mpya za matumizi ya ardhi zilizochapishwa kwenye Gazeti la Serikali la Aprili mwaka huu, pia imekuja na masharti mapya ya matumizi ya mikopo ya kuendeleza ardhi inayopatikana kwa kutumia dhamana ya ardhi ya Tanzania.

Kwa mujibu wa kanuni hiyo inayosaidia utekelezaji wa mabadiliko ya Sheria ya Ardhi yaliyofanywa na Bunge mwaka jana, wakopaji katika benki za nje au ndani wanaotumia dhamana ya ardhi, lazima wawasilishe kwa kamishna wa ardhi tamko kuwa fedha hizo zitawekezwa Tanzania pekee.

Kanuni hizo zinawataka wakopaji pia kuwasilisha kwa kamishna, ripoti ya matumizi ya fedha walizokopa ndani ya miezi sita baada ya kupata mikopo hiyo.

Masharti hayo mapya yamekuja wakati Serikali ikieleza kutoridhika na namna mabilioni ya shilingi ya yaliyopatikana kutoka benki za nje na ndani kwa maendeleo ya ardhi kutumia dhamana ya ardhi nchini ambayo yamechepushwa kwenye shughuli zisizohusiana na uendelezaji wa ardhi.

Chanzo vya habari katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kimesema, Serikali imepata changamoto kubwa kutengua hati za umiliki wa mashamba yaliyotumika kukopa fedha kutoka benki za nje.

Waziri wa Ardhi, William Lukuvi akizungumza na Mwananchi hivi karibuni alisema kununi hizo mpya hazijamlenga mtu, bali zimekuja kuweka msingi wa matumizi mazuri ya rasilimali ya Taifa.

Alisema uchepushaji wa fedha zilizolenga kuendeleza ardhi zimeinyima Serikali Kuu, Serikali za wilaya na viji, mabilioni ya kodi na kuondoa ndoto ya ajira kwa vijiji vilivyotoa ardhi kubwa za shuguli za uwekezaji.

Kuna watu wamechukua ardhi kubwa wakaikopea fedha na wakawa matajiri na kuwaacha wanavijiji waliokaa vikao kuruhusu ardhi yao itumike kwa masharti ya wao kunufaika katika umaskini mkubwa.

“Mtu anachukua Dola 20 millioni za kuendeleza ardhi kutoka benki ya nje kwa kutumia ardhi yetu, lakini ukienda shambani hakuna kilichofanyika. Sasa hizo fedha zimekwenda wapi na ardhi yetu imewekwa dhamana nje,” alihoji Waziri Lukuvi.

Kwa mujibu wa kanuni hizo mpya, watu wanaokopa fedha kwa kutumia dhamana ya ardhi isiyoendelezwa kabisa au iliyoendelezwa kiasi, watalazimika kuingiza fedha zote au kiasi katika ardhi husika na si vinginevyo.

Hata hivyo, kanuni hizo zinatoa mwanya kwa wakopaji wa kutumia dhamana ya ardhi kutumia fedha za mkopo kwa shughuli nyingine yoyote endapo ardhi wanayotumia kukopea imekwishaendelezwa.

Wachumi na wataalamu wa masuala ya ardhi wamepongeza ujio wa sheria na kununi hizi, wakisema zilikawia mno.

“Watu wengi wamepata utajiri mkubwa kwa kukopea mashamba yetu. Kama itatumika ipasavyo, itasaidia wanaotaka kukopa kuendeleza mashamba pori na hivyo kuongeza ajira na kukuza kipato na uchumi wa watu,” alisema Ofisa Programu Mwandamizi wa HakiArdhi, Joseph Chiombola .

Hata hivyo, alionyesha wasiwasi wa jinsi gani Serikali itakavyohakikisha kuwa fedha za mikopo ya mashamba itatumika kwa kusudi husika.

Mchumi maarufu na mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba alisema anaunga mkono sheria na kanuni hizo mpya.