Mawakili kesi ya Mpemba wa Magufuli waibua jambo

Muktasari:

Upande wa utetezi kesi ya Yusuf Ali maarufu ‘Mpemba wa Magufuli' na wenzake, umeieleza mahakama kuwa upande wa mashtaka unajichanganya.

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi Yusuf Ali maarufu ‘Mpemba wa Magufuli' na wenzake, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upande wa mashtaka unajichanganya kuhusu wanasheria  wa Serikali.

Yusuf na wenzake watano, wanakabiliwa na mashtaka manne katika kesi ya Uhujumu Uchumi likiwemo la kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh785.6milioni.

Hayo yameelezwa na wakili wa utetezi, Haisan Kiangio mbele ya Hakimu Mwandamizi, Augustina Mmbando baada ya wakili wa Serikali, Tully Helela kudai kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.

Kauli ya wakili wa Serikali, Helela ilimshangaza Kiangio  aliyedai kuwa upande wa mashtaka wanajichanganya kwani wanaokuja kwenye kesi hiyo ni wanasheria tofauti.

Kiangio amedai kauli ya mwisho ya wakili wa Serikali mwandamizi, Faraja Mchimbi aliieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi umekamilika na wanatarajia kupeleka taarifa Mahakama Kuu.

"Jamhuri inajichanganya wanakuja mawakili wa Serikali tofauti tofauti hawajui mara ya mwisho kiliongelewa kitu gani katika shauri hilo," amedai Kiangio.

Hakimu Mmbando ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 25, 2019 itakapotajwa tena na washtakiwa wamerudishwa rumande kwa kuwa mashtaka yao hayana dhamana.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Charles Mrutu, Benedict Kungwa, Jumanne Chima, Ahmed Nyagongo na Pius Kulagwa.

Katika kesi ya msingi, tarehe tofauti kati ya Januari 2014 na Oktoba 2016 wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola 180,000 za Marekani sawa na Sh392.8milioni bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.