VIDEO: Mbunge, RC watuhumiana kwa rushwa mbele ya mawaziri

Monday July 29 2019

By Joseph Lyimo, Mwananchi [email protected]

Mirerani. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti na Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya wamerushiana maneno hadharani wakituhumiana rushwa na kuwatishia wachimbaji wa madini kwa silaha ili kupata fedha.

Tukio hilo limetokea jana mjini hapa wakati kamati ya kuchunguza na kutatua migogoro ya mpaka baina ya kampuni ya TanzaniteOne na wachimbaji wadogo wa Kitalu B na D ilipokuwa ikisoma taarifa yake mbele ya Waziri wa Madini, Dotto Biteko kwenye mkutano wa hadhara.

Ole Millya alisema mkuu huyo wa mkoa anapaswa kukaa mbali na TanzaniteOne akidai wanampa fedha ili awatetee, ndiyo sababu anatoa amri nyingine za kuwakwamisha wachimbaji wadogo kwa kuwataka walipe mishahara jambo ambalo haliwezekani.

“Kuna habari zinaenea eti yupo karibu na viongozi wakuu wa nchi, kwa hiyo akipingwa mimi nitapoteza ubunge, wacha nipoteze, sipo tayari kuona wachimbaji wadogo wakinyanyaswa kwa masilahi ya wachache,” alidai Millya.

Alisema atasimama kidete na wananchi na ndiyo sababu hata katika Kata ya Kitwai kuna mfugaji anaingiza mifugo yake akitetewa na viongozi na anapoingilia kati anaambiwa ataundiwa tume kupitia kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kwa ajili ya kuchunguzwa.

Wakati Milya akidai hayo, Mnyeti naye alisimama na kusema anasikitika kutuhumiwa na mbunge huyo wakati siku zote husimama kidete kuwatetea wachimbaji wadogo ambao kwa kiasi kikubwa wananyanyasika kutokana na kutolipwa mishahara.

Advertisement

“Nataka kukuhakikishia (Millya), mimi sina njaa. Kabla ya kuwa mkuu wa mkoa nilikuwa wa mkuu wa wilaya, nipo vizuri huwezi kuniambia nisiwe karibu na wawekezaji wa TanzaniteOne ili hali ni walipaji wakubwa wa kodi.

“Nimepata malalamiko kuwa wewe mbunge unawatishia watu na bastola ukitaka wachimbaji wa madini wakupe fedha badala ya kujibu hilo, unanitukana hadharani kuwa nimepewa fedha na kampuni ya uchimbaji madini au niwataje hadharani?” alihoji Mnyeti na kujibiwa na Millya wataje.

Kwa taarifa Zaidi Usikose Gazeti la Mwananchi la Julai 29, 2019. Pamoja Kutizama Video hii

Advertisement