VIDEO: Mbunge Bonnah ‘Kaluwa’ akiri ndoa yake kuvunjika

Tuesday February 26 2019

 

By Mwandishi wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Mbunge wa Segerea (CCM) jijini Dar es Salaam aliyekuwa akitumia jina la Bonnah Kaluwa amekiri kuachana na mume wake Moses Kaluwa na hivyo kulazimika kubadili majina.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Februari 26,2019 mbunge huyo wa CCM ambaye kwa sasa anatumia jina la Bonnah Kamoli, amesema amebadilisha majina yake katika mitandao ya jamii.

Hata hivyo, tovuti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kutumia majina yake ya a wali ya ‘Bonnah Moses Kaluwa.’

“Taarifa ni za kweli tumeachana,” amesema Bonnah kwa njia ya simu.

Alipoulizwa sababu ya kufikia hatua hiyo, Bonnah amesema, “Ni matatizo ya kifamilia.”

“Nimeshaweka majina yangu kwenye mitandao ya kijamii. Nimeweka Instagram, Facebook. Bunge wana taratibu zao, si wamepata barua? Mimi nimepata yangu nimebadilisha,” amesema.

Advertisement

Kampuni ya uwakili ya Carmel Attorney inayomsimamia aliyekuwa mume imethibitisha kumwandikia barua na nyingine kupeleka Bungeni kumzuia kutumia jina la Kaluwa.

Mmoja wa mawakili wa kampuni hiyo ambaye hakutaka jina liandikwe gazetini amesema suala hilo lilitokea tangu Novemba 2018, lakini bado hawajafuatilia kama agizo lao limetekelezwa.

“Ni kweli huyo ni mteja wetu alikuja hapa tukaandika barua na kupeleka Bungeni na nyingine kwa Bonnah. Bado hatujafuatilia kwa sababu mteja wetu hajaja tena kulalamika,” amesema Wakili huyo.

Hata hivyo, amesema suala hilo ni la siku nyingi na hawakutaka kuliweka wazi ili kulinda heshima ya Bonnah ambaye ni Mbunge.

“Hayo mambo ni ya siku nyingi, mteja wetu alitaka tusitoe hadharani ili kulinda hadhi ya Mbunge. Sasa inawezekana yeye mwenyewe ndiyo anayasambaza. Wameshapeana talaka siyo kwamba kuna dalili za usuluhishi,” alisema.

 Advertisement