Mbunge Chadema amtaka Profesa Kabudi ajiuzulu

Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema) Anthony Komu akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu amemtaka Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba  Kabudi kujiuzulu kwa madai kuwa ameitia Serikali ya Tanzania hasara

Dodoma. Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu amemtaka Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba  Kabudi kujiuzulu kwa madai kuwa ameitia Serikali hasara.

Akizungumza leo Jumatano Mei 15, 2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara mwaka 2019/2020, mbunge huyo amesema maamuzi ya Profesa Kabudi yamekuwa shida kwa Taifa.

Kabla ya kuteuliwa kuongoza wizara ya Mambo ya Nje, msomi huyo alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

"Profesa Kabudi ndiyo tatizo kwa nchi hii, ameliingiza Taifa kwenye matatizo makubwa kwa mfano kwenye korosho, sheria ya takwimu, Mpango wa PPP, makinikia na mengine mengi tu," amesema Komu.

Mbunge huyo amelitaka Bunge kuchukua hatua za kumwajibisha waziri huyo kwa kuwa anafanya uamuzi wa kuwadanganya Watanzania.

Pia amesema kwamba Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga na Waziri wa Viwanda, Joseph Kakunda wapo lakini hawajui kinachoendelea.