Mbunge ahoji matukio ya wapinzani kutoonyeshwa, Dk Tulia amtuliza

Sophia Mwakagenda

Muktasari:

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Sophia Mwakagenda ameilalamikia Televisheni ya Taifa (TBC) kwa kutorusha habari za upinzani

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Sophia Mwakagenda amelalamikia kile alichokiita ubaguzi unaofanywa na Televisheni ya Taifa (TBC) kwa kutorusha habari za upinzani.

Akizungumza bungeni leo Jumatano Mei 15, 2019 Mwakagenda amesema TBC imekuwa na ubaguzi wa kutoa habari za wapinzani na kwamba kila wakati wamekuwa wakitoa habari zinazowahusu wabunge wa upande mmoja wakati ni chombo cha Serikali.

Akijibu mwongozo wa Mwakagenda, naibu Spika, Dk Tulia Ackson ameiomba Serikali kulitazama jambo hilo huku akibainisha kuwa hata taarifa za wabunge wa CCM wakati mwingine hazitoki na badala yake hutoka za upinzani pekee.

“Jana niliuliza swali kwa Waziri wa Mawasiliano lakini Waziri wa habari alijibu, hii TBC ni mali ya walipa kodi lakini imekuwa haitendi haki, kila wakati sisi wapinzani tunabaguliwa kwa habari zetu kutotumika tatizo ni nini,” amehoji Mwakagenda.

Mbunge huyo ametolea mfano hotuba za upinzani na michango yao kwamba kila wakati hakuna kinachotolewa kwenye televisheni hiyo akisema hakuna usawa.

Katika ufafanuzi wake Dk Tulia  amesema jambo hilo lilitokea jana hivyo liko kinyume na kanuni za Bunge ambazo hutaka jambo lililotokea mapema ndio kuulizwa bungeni.