Mbunge ataka kutoa Sh1 milioni kuiepushia aibu Serikali

Muktasari:

  • Mbunge wa Baraza la Wawakilishi (CCM) Jaku Hashim Ayoub amezungumzia kuhusu uchakavu wa vituo vya polisi Zanzibar na kuhoji Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo vipya.

Dodoma. Mbunge wa Baraza la Wawakilishi (CCM) Jaku Hashimu Ayoub amesema kumekuwa na kilio cha uchakavu wa vituo vya polisi upande wa Zanzibar na kusababisha askari kufanya kazi katika mazingira magumu hasa katika vipindi vya jua kali au mvua.

“Je ni vituo vingapi vipya vya polisi vilivyojengwa kwa upande wa Unguja na Pemba?” amehoji mbunge huyo bungeni leo Jumanne Aprili 16 mwaka 2019.

Jaku amehoji pia vituo hivyo vimejengwa na kampuni gani na ni vigezo gani vilivyoangaliwa katika ujenzi wa vituo hivyo.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema vituo vingi vimejengwa au kukarabatiwa katika miaka tofauti ikiwemo vituo vya Mwembe Madafu na Mbweni katika mkoa wa Mjini Magharibi.

Vingine ni Kituo cha Mchanga Mdogo Mkoani Kaskazini Pemba, vituo vya Chwaka na Jambiani mkoa wa Kusini Unguja, Chakechake na Mtambile vilivyopo mkoa wa Kusini Pemba.

“Kuna ujenzi unaendelea kwa sasa wa vituo vya Chukwani, Dunga na Mkokotoni,” amesema Lugola.

Amesema ujenzi wa vituo vingi vya polisi ulikuwa ni ushirikiano wa wananchi na Jeshi la Polisi.

Amesema mkandarasi MS Albatina Construction Company Ltd anayejenga kituo cha Polisi Mkokotoni, anaendelea na kazi yake.

Katika swali la nyongeza Ayoub amesema deni wanalodaiwa Serikali na mkandarasi anayejenga vituo vya polisi Zanzibar ni la muda mrefu na ni aibu.

“Aibu kwa Serikali kupata deni hilo. Mimi niko tayari kuchangia milioni moja kupeleka hapa ili kulipa deni hili. Je upo tayari kufuatana nami kupeleka hii,” amesema huku akionyesha fedha hizo.

Akijibu swali hilo, Waziri Lugola amesema utaratibu wa ujenzi wa vituo hivyo unahusisha wadau mbalimbali na kumtaka mbunge huyo kupeleka fedha hizo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro.

“Ni kweli deni hili ni la siku nyingi. Jaku ni mbunge king’ang’anizi na moto wa kuotea mbali anapolifuatilia jambo,’’ amesema.

Naye mbunge wa Chemba (CCM) Juma Nkamia alihoji kuhusu kituo cha polisi Chemba, “Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi pale Chemba.”

Akijibu swali hilo, Lugola amesema Jeshi la Polisi lina mikoa ya kipolisi 35, wilaya za kipolisi 182 na tarafa 610.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma hizo  zinaenda kote na kwamba huko Chemba ni miongoni wa maeneo watakakokwenda.