Mfuko mdogo wa plastiki kukuweka jela siku saba, faini ya Sh30,000

Zimesalia siku nane kabla ya kuanza kwa marufuku ya mifuko ya plasitiki nchini.

Marufuku hiyo inahusisha kuzalisha, kuagiza, kusafirisha nje ya nchi, kuhifadhi, kusambaza, kuuza, kumiliki na kutumia mifuko ya plastiki katika eneo lote la Tanzania bara.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi Aprili mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba alisema utekelezaji wa marufuku hayo utaanza kutumika Juni Mosi mwaka huu.

Makamba aliwataka watumiaji, wazalishaji, wasafirishaji na wafanyabiashara wanaotumia mifuko ya plastiki kujiandaa kuachana nayo badala yake wajielekeze katika matumizi ya mifuko au vibebeo mbadala ambavyo ni rafiki kwa mazingira.

Changamoto kubwa inayotajwa katika mifuko ya plastiki ni athari zake kwa mazingira na hata kwa maisha ya binadamu, wanyama na uchumi.

Katika kuelekea utekelezaji wa marufuku hiyo, Serikali imechapisha katika gazeti la Serikali, sheria na kanuni zinazohusiana na marufuku dhidi ya mifuko ya plastiki.

Kupitia Makala hii tunakuletea kwa muhtasari mambo muhimu yaliyomo kwenye kanuni hizo zilizochapishwa kwenye gazeti la Serikali Mei, 17 mwaka huu;

Makosa matano

Makosa matano yaliyotajwa na kukatazwa ndani ya sheria hiyo ndogo inayojulikana kama The Environmental Management (Sheria ya Usimamizi wa Mazingira) ‘Prohibition of Plastic Carrier Bags’ (udhibiti mifuko ya plastiki) ya mwaka, 2019 ambayo imetungwa kwa mujibu wa Kifungu Na. 230 (2) (f) cha Sheria inayojihusisha na usimamizi wa Mazingira (The Environmental Management Act, Cap. 191).

Kifungu au Kanuni Na. 8 cha Sheria ya kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki, 2019 kinayataja makosa hayo ni kuzalisha na kuagiza, kusafirisha nje ya nchi, kuhifadhi na kusambaza, kuuza na kumiliki na kutumia mifuko ya plastiki.

Kwa mujibu wa sheria na kanuni hizo, kwa kila kosa sheria husika imetaja adhabu yake. Hivyo basi kuna aina tano za adhabu kama ilivyo kwa makosa husika.

Inasena adhabu kwa wazalishaji na waagizaji ni faini isiyopungua Sh20 milioni na isiyozidi Sh1 billioni, kifungo kisichozidi miaka miwili au vyote yaani kifungo na faini.

Kwa upande wa wasafirishaji nje ya nchi adhabu yao ni faini isiyopungua Sh5 milioni na isiyozidi Sh20 milioni, kifungo kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.

Adhabu kwa wanaohifadhi na wasambazaji ni faini isiyopungua Sh5 milioni na isiyozidi Sh50 milioni, kifungo kisichozidi miaka miwili au vyote yaani kifungo na faini vinaweza kutolewa kwa pamoja.

Kwa upande wa wauzaji kanuni za sheria hiyo zinasema mtu au watu watakaotiwa hatiani wanaweza kutozwa faini isiyopungua Sh100,000 na isiyozidi Sh500,000, kifungo kisichozidi miezi mitatu au vyote kwa pamoja.

Pia, inasema adhabu kwa watumiaji na wanaomiliki adhabu yao ni faini isiyopungua Sh30,000 na isiyozidi Sh200,000, kifungo kisichozidi siku saba au muhusika anaweza kuadhibiwa na vyote hivyo kwa pamoja.

Kanuni hizo zinatamka kuwa sheria hiyo itahusisha mifuko yote ya plastiki ama iwe inayotengenezwa nchini au kuagizwa kutoka nje ya nchi kama haipo katika kundi la vifungashio vya plastiki vilivyopewa msamaha kisheria.

Bidhaa zilizosamehewa

Sheria na kanuni hizo zinasema baada ya kuanza kutumika kwa sheria hiyo hakuna mamlaka itakayotoa leseni au kibali kwa yeyote atakayetaka kuingiza au kusafirisha mifuko ya plastiki ambayo imepigwa marufuku na kwamba atakayekutwa akifanya hivyo atachukuliwa hatua.

Kwa mujibu wa sheria na kanuni hizo, bila ya kuathiri vifungu vingine inaelezwa kuwa vimepewa msamaha vibebeo na vifungshio vinavyotumika kwa ajili ya huduma za matibabu, bidhaa za viwandani, ujenzi, sekta ya kilimo na uandaaji wa chakula ambavyo vimeondolewa katika marufuku hiyo.

Hata hivyo, yeyote anayeingiza, kusafirisha, kuuza, kuhifadhi, kusambaza, kumiliki au kutumia moja ya vifungashio vilivyo katika orodha ya msamaha kuhakikisha baada ya matumizi vinaharibiwa kulingana na sheria na kanuni za mazingira zinavyotaka.

Mbali na hilo, wote wanaoingiza na kusafirisha bidhaa za vibebeo na vifungashio vya plastiki vilivyo katika kundi la msamaha kuhakikisha zinazingatia ubora kama inavyoelekezwa na Shirika la Viwango (TBS).

Kanuni hizo zinasema waziri mwenye dhamana ya mazingira wakati wowote atakaoona unafaa anaweza kutoa maelekezo na miongozo kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa kanuni hizo.

Aidha, waziri kwa kushirikiana na waziri mwenye dhamana ya fedha wataendelea kuhamasisha utengenezwaji wa mifuko mbadala itakayotumika baada ya kuondoka kwa mifuko plastiki.

Fursa ya ajira

Baadhi ya wenye viwanda wanasema marufuku hiyo inaweza kuwa fursa kwa kutengeneza mifuko mbadala na kuzalisha ajira na kipatano.

Miongoni mwa wanaoitazama hatua hiyo kama fursa ni Pius Nyomolelo wa kiwanda cha vifungashio mkoani Iringa, anayesema kuzuiliwa kwa mifuko ya plastiki ni fursa kwao kwani ilikuwa ikiwanyima soko la bidhaa zao.

Kuhusu malighafi anasema, “awali tulikuwa tunanunua karatasi Dar es Salaam, lakini tunamshukuru Rais John Magufuli tangu alipokwenda katika kiwanda cha Mgololo aliagiza tupewe, kwa hiyo tunazipata huko sasa.”

Fursa hiyo ipokewe na kufanyiwa kazi na kila mmoja kwa nafasi yake ili kuondoa pengo litakalosababishwa na kuondoka kwa mifuko hiyo.

Huko nyuma kuliwahi kuwa na viwanda vingi vidogovidogo vilivyokuwa vikitengeneza vibebeo wakati huo ikijulukana kama mifuko ya karatasi au ya kaki. Viwanda hivyo vinaweza kuanzishwa sasa na kuwa msaada katika uzalishaji ajira.