Breaking News

Miamala ya M-pesa hata kama huna salio

Friday July 12 2019

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kampuni ya huduma za simu ya Vodacom Tanzania kwa kushirikiana na benki ya TPB wameanzisha huduma itakayowawezesha watumiaji wa huduma za M-Pesa kukamilisha miamala hata kama hawana salio la kutosha katika akaunti zao.

Huduma hiyo ambayo ipo chini ya idara ya M- Commerce inayosimamia pia, ilitangazwa juzi katika mkutano na waandishi wa habari, makao makuu ya Vodacom jijini Dar es Salaam Tanzania.

Katika mkutanao huo, Mkurugenzi wa M-Commerce, Epimack Mbeteni alisema walichunguza vikwazo vya mara kwa mara kwa wateja wao kukamilisha miamala, ndipo wakaja na suluhisho hilo ambalo litasaidia kukamilika kwa miamala ambayo awali isingekamilika kwa sababu ya upungufu wa fedha.

 “M-Pesa Songesha ni moja kati ya huduma nyingi za M-Commerce zilizozinduliwa mwaka huu, Tumeungana na benki ya TPB kuwezesha huduma hii na ili kuamua kiwango mteja anachostahili, benki itatumia taratibu zilizowekwa kulingana na miamala ya mteja husika katika matumizi yake ya M-Pesa,” alisema Mbeteni.

Watumiaji wa M-Pesa wanaweza kufikia Songesha kwa kupiga namba za huduma ya MPesa, *150*00#, kisha kuchagua huduma za kifedha na kujiunga na huduma hiyo ya M-Pesa Songesha. Mara tu baada ya mteja kujiunga na Songesha, atapata ujumbe wa kiwango ambacho anastahili na ataweza kutumia kiwango hicho kukamilisha miamala yake. Kiasi hicho kitarejeshwa pale ambapo mteja atapokea fedha katika akaunti yake ya M-Pesa.

Alisema baada ya mteja kujiunga na huduma hiyo atapata ujumbe wa kiwango anachostahili na marejesho ya fedha iliyozidi itakatwa pale mteja atakapopokea fedha katika akaunti yake ya Mpesa, "Kiwango hicho kina riba ya asilimia 1 kwa siku 18”.

Advertisement

Kaimu Afisa mtendaji mkuu wa TPB Moses Manyatta alisema benki imeingia ushirika huo ili kuhamasisha huduma jumuishi za kifedha na kuwahamasisha watanzania kuwa na tabia ya kuweka akiba.

“Songesha inapatikana masaa 24 kwa siku saba tuna Imani mapinduzi haya yatasaidia katika huduma jumuishi za kifedha,” alisema Manyatta.

Advertisement