Mikuni; Mlemavu wa macho aliyekataa kuwa ombaomba

Watu wengi huamini kuwa utafutaji wa kipato hususani cha kiuchumi unamhusu zaidi binadamu aliye na viungo timilifu. Fikra hizo hujenga imani kuwa siku zote wenye ulemavu ni watu wenye kuhitaji msaada na kusaidiwa tu.

Dhana hiyo iko tofauti kabisa na mawazo ya Mikuni Mikuni (35), mlemavu wa macho anayetembea kwa msaada wa fimbo maalumu zinazotumiwa na wasioona, lakini fikra zake zinaweza kuwa zimepevuka kuliko hata baadhi ya watu wenye utimamu wa viungo.

Mikuni ambaye ni baba wa watoto wa wawili, kwake kuomba ni mwiko, licha ya ulemavu alionao anaamini kuwa anatakiwa kufanya kazi ili aweze kupata kipato kitakachomwezesha kukidhi mahitaji ya familia yake.

Licha ya elimu yake ya darasa la saba, Mikuni anaamini anaweza kuishi bila ya kuwa tegemezi kwa kuwa viungo vingine vya mwili wake viko sawa, hivyo siku zote atafanya kazi na kusimama kama baba wa familia.

Kijana huyo mkazi wa Kijiji cha Kise, Kata ya Kiparang’anda wilayani Mkuranga ni taswira halisi ya walemavu ambao wanafahamu kuwa ulemavu si sababu ya kumfanya mtu awe tegemezi.

“Nimeshajiapiza kwenye maisha yangu kuomba ni mwiko, msaada nitakaohitaji ni kuwezeshwa nifanye kitu fulani, lakini sio kila siku nikae barabarani kusubiri wapita njia niwaombe fedha.

“Sipendi watoto wangu wanung’unike pale wanapokosa kitu na kuhusisha na ulemavu wangu, hivyo najitahidi wapate mahitaji yote muhimu, wasome hadi chuo kikuu na tayari wa kwanza ameshaanza sekondari hii ni dalili njema,” anasema Mikuni.

Pamoja na ulemavu wake wa macho Mikuni anajihusisha na ufugaji kuku wa kienyeji kwa kushirikiana na mke wake ambaye ni mama lishe na wote kwa pamoja wanatengeneza fedha kwa ajili ya familia yao.

Changamoto kubwa aliyonayo ni ulinzi wa mifugo hiyo mke wake asipokuwepo nyumbani, kwani watu wasiokuwa na nia njema huiba kuku wao na kupunguza idadi yao siku hadi siku.

Mikuni ni miongoni mwa vijana 60 waliopata mafunzo ya ujasiriamali yaliyotolewa na asasi ya Social Information and Facilitation (Sifo), kupitia mradi wa Paza Sauti yaliyohusisha kata sita za wilaya ya Mkuranga.

Hakujali ulemavu wake, katika kipindi chote cha mafunzo, Mikuni alishirikiana na wenzake kutengeneza bidhaa mbalimbali na wakati mwingine alijaribu kufanya peke yake ili kupima uwezo wake.

Mafunzo hayo yalimuwezesha kujifunza kutengeneza batiki, mikoba na viatu vya shanga, dawa za kusafishia chooni na sabuni za miche na za unga.

“Unaweza usiamini kwa sababu sina macho ila ninachoweza kusema masikio yangu yalikuwa makini mno kwa kila lililofundishwa na hapa nilipo naweza kutengeneza baadhi ya bidhaa.

“Hamu yangu kubwa ilikuwa kujifunza kutengeneza mikoba ya shanga na batiki vitu ambavyo nimeviweza kuvifanya kwa mikono yangu, sasa najikita kutafuta mtaji nianzishe rasmi shughuli hii. Nafahamu kuwa bidhaa zinazohusisha wanawake zina soko kubwa,” anasema.

Mikuni anawasisitiza walemavu wengine kujikita katika kutafuta fursa na si misaada kwani hiyo haiwezi kudumu bali wataishia kuwa ombaomba wakati wana nguvu za kufanya kazi.

Pia, ameziomba asasi za kiraia na taasisi za Serikali zinazotoa mafunzo kuwatafuta walemavu ili wawe sehemu ya kupata ujuzi na kuutumia katika kujikwamua kimaisha.

Mratibu wa mradi huo, Hashim Mohamed anamtaja Mikuni kama kijana mwenye ari kubwa ya kujifunza vitu vipya na kutaka kujaribu bila kukatishwa tamaa na hali aliyonayo.

Anasema kwamba mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo vijana waliopo kwenye majukwaa na kuwawezesha kufanya kazi za mikono na kuzitumia kama fursa ya kujiingizia kipato badala ya kulalamikia ukosefu wa ajira.

“Sisi tunaamini kijana ukimpa nyenzo anaweza kufanya vizuri kuliko kumpa fedha na huu ujuzi walioupata watautumia katika maisha yao yote na kujikwamua dhidi ya umaskini, hilo ndilo jambo ambalo Mikuni analisimamia,” anasema.

Anasema kwamba kupitia ufadhili wanaoupata kutoka Mfuko wa Asasi za Kiraia (FCS) siku zote wamekuwa wakiwahusisha watu wenye ulemavu katika shughuli zao kwa kuwa wanaamini kundi hilo limetengwa ila linaweza kufanya vizuri endapo litapewa nafasi.