Mke atuhumiwa kumuua mumewe kwa bisibisi

Tuesday August 6 2019

 

By Sanjito Msafiri, Mwananchi [email protected]

Pwani. Polisi Mkoa wa Pwani nchini Tanzania linamshikilia Mwajuma Malembeka mkazi wa Kijiji cha Chamalole wilayani Kisarawe mkoani humo kwa tuhuma za kumuua mumewe Selemani Kondo Selemani.

Taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Wankyo Nyigesa  aliyoitoa jana Jumatatu Agosti 5, 2019 kwa wanahabari ilisema mtuhumiwa huyo anadaiwa kumuua mumewe Ijumaa iliyopita ya Agosti 2, 2019 kwa kumchoma bisibisi kwenye bega la mkono wa kulia.

Nyigesa alisema chanzo cha ugomvi huo kinadaiwa ni wivu wa mapenzi ambapo mwanamke huyo alimtuhumu Selemani kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine.

Kamanda huyo alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

Advertisement