Mkutano wa SADC wawarejesha Tanzania mabalozi 42

Tuesday August 13 2019

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbasi amesema tayari mabalozi 42 wa Tanzania wanaowakilisha katika nchi mbalimbali duniani wamewasili nchini kushiriki Mkutano wa 39 wa Wakuu na Serikali katika Nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika(SADC).

Dk Abbasi amesema kabla ya mkutano huo, mabalozi hao kesho Jumatano watembelea mradi wa uzalishaji umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), unaotekelezwa katika mto Rufiji kwa ajili ya kuzalisha megawati 2,155.

Akizungumza na wanahabari leo Jumanne Agosti 12, 2019 Jijini Dar es Salaam, Dk Abbas amesema ziara ya kutembelea mradi huo ni kukusanya taarifa zitakazowasaidia kujenga uwezo wakushawishi mazingira ya uwekezaji Tanzania.

“Kesho pia Tanzania tutampokea Rais wa Afrika Kusini, Cyill Ramaphoza kwa ajili ya kuanza ziara ya kitaifa ya siku tatu, itaanza kesho jioni hadi Agosti 16, pia atatembelea eneo la kihistoria Mazimbu, Morogoro lililotumika kusaidia ukombozi wa bara la Afrika.”

“Kwa hiyo viongozi wengi wa kusini mwa Afrika, si tu kwamba wanakuja katika mkutano ila wanarudi nyumbani na viongozi wote wamethibitisha kushiriki katika mkutano huo mkuu,” amesema Dk Abbas ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Itifaki ya SADC, kila balozi kwa sasa atakuwa ni mwenyekiti wa kamati ya mabalozi wa Nchi za SADC, ndani ya nchi husika anayowakilisha.

Advertisement

Advertisement