Mnyika ahoji Serikali kutotenga fedha za kura ya maoni

Mbunge wa Kibamba, John Mnyika akichangia bungeni mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Bunge la Katiba lilikamilisha kazi yake ya kuandika Katiba mpya  kwa kukamilisha upigaji wa kura za kupitisha Rasimu ya Katiba ambayo ilitakiwa ipitishwe kwa kura ya maoni kwa theluthi mbili ya kura kutoka kila upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini mchakato wa kupiga kura hiyo ulisimama kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Dodoma. Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika ameitaka Serikali kueleza sababu za kutotenga fedha kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa kura ya maoni kupitisha Katiba inayopendekezwa.

Mnyika ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) mwaka 2019/2020.

Mbunge huyo amesema hata Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inaeleza kuwa kipaumbele cha chama hicho tawala ni Katiba mpya.

“Tumeapa kulinda Katiba naelewa wenzetu tukisema kuhusu Katiba mnasema kipaumbele cha wananchi ni maji, umeme na miradi mingine ya maendeleo.”

“Katiba ndio nyenzo ya kusimamia mambo yote na ndio nyenzo ya kuleta maendeleo ya wananchi, kwa sababu ni jambo la pili muhimu kwa nchi yetu, niwakumbushe Rais  (John Magufuli) wakati akizindua Bunge aliahidi ataendeleza na kukamilisha mchakato wa Katiba mpya,” amesema.

Mnyika amedai siku za hivi karibuni Rais Magufuli akiwa katika kongamano Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) alisema hataki mchakato wa Katiba kuendelea kwa sababu watu wanataka kupewa posho bungeni.

“Ofisi ya Rais imkumbushe kwamba hatua iliyofuata ni kura ya maoni kupitisha Katiba mpya, ni muhimu katika majumuisho ofisi ya Rais ikasema kwanini katika bunge hili haijatengwa fedha kwa ajili ya kura ya maoni na kupitisha Katiba.”

“Ilani ya uchaguzi ya CCM inasema bayana kuwa CCM itaendeleza na kukamilisha mchakato wa Katiba tekelezeni Ilani yenu,” amesema Mnyika.

Kauli hiyo ilimnyanyua mbunge wa Kibakwe (CCM), George Simbachawene ambaye amesema: “Katiba inayopendekezwa tulishiriki wabunge wote na mchakato ulipofikia hatua fulani wenzetu wa upinzani walikataa, wanatakaje sasa Katiba wakati hawakushiriki hadi mwisho?”

Akijibu taarifa hiyo Mnyika amesema: "Sheria  ya kura ya maoni inasema ikipitishwa na Bunge la Katiba hatua inayofuata ni kura ya maoni.”