Mnyika aibua sakata la CAG bungeni, Chenge amtuliza

Mbunge wa Kibamba, John Mnyika akiomba mwongozo bungeni leo alipokuwa akihoji sababu za orodha ya shughuli za Bunge kutoonyesha kama taarifa ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali itawasilishwa bungeni, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika amehoji sababu ya orodha ya shughuli za Bunge leo Jumatatu Aprili 8, 2019 kutoonyesha kuwasilishwa kwa taarifa ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Dodoma. Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika ameomba mwongozo bungeni akihoji sababu ya orodha ya shughuli za leo bungeni Aprili 8, 2019 kutoonyesha kuwasilishwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad, akidai ni kinyume na Katiba.

Mnyika alitumia kifungu cha 143 (4) cha Katiba ya Tanzania kuomba mwongozo huo, lakini mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama wamemtaka mbunge huyo kusoma vyema sheria na tafsiri ya sheria ili kuelewa kwa kina muda wa uwasilishwaji wa taarifa hiyo bungeni.

Ibara ya 143 (4) inasema; Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atawasilisha kwa Rais kila taarifa atakayotoa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2) ya ibara hii.  Baada ya kupokea taarifa hiyo Rais atawaagiza watu wanaohusika wawasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha kwanza cha Bunge kitakachofanyika baada ya Rais kupokea taarifa hiyo na itabidi iwasilishwe katika kikao hicho kabla ya kupita siku saba tangu siku ile kilipoanza kikao hicho.  Iwapo Rais hatachukua hatua za kuwasilisha taarifa hiyo kwa Spika wa Bunge (au Naibu wa Spika ikiwa kiti cha Spika ki wazi wakati huo au ikiwa kwa sababu yoyote Spika hawezi kutekeleza shughuli za kazi yake) ambaye atawasilisha taarifa hiyo kwenye Bunge.

Mnyika amesema, “Mapema leo asubuhi tumekabidhiwa orodha ya shughuli za leo ambayo pamoja na mambo mengine kulikuwa na hati za kuwasilishwa mezani, lakini mwenyekiti Katiba 143 (4) inasema CAG atawasilisha kwa Rais (na kusoma ibara hiyo).”

“Naomba mwongozo wako kwa sababu taarifa iliyotolewa na CAG inaonyesha kwamba Machi 28, 2019 Rais alipokea ripoti za ukaguzi kutoka kwa CAG kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2018, na kikao cha kwanza cha Bunge kilianza Aprili 2, 2019 na taarifa (za CAG) zilizowasilishwa kwa Rais hazikuwasilishwa hadi sasa (bungeni),” amesema Mnyika.

“Katiba haikusema kama ni siku saba za kazi ama zisizokuwa za kazi. Kwanini orodha ya shughuli za Bunge leo hakuna ripoti ya CAG katika hati zilizowasilishwa mezani.”

Amehoji kwa nini orodha hiyo ya shughuli za Bunge isibadilishwe iletwe inayoonyesha orodha ya shughuli, “na kama hailetwi hiyo ni tarehe ngapi Rais ataagiza iletwe orodha ya CAG bungeni kabla ya muda (wa siku saba).”

Baada ya Mnyika kuomba mwongozo huo Mhagama alisimama na kuomba mwongozo, akitoa ufafanuzi kuhusu hoja ya Mnyika, “Kwa kuwa katika mijadala iliyoendelea bungeni leo, Mnyika wakati akiomba mwongozo ameonyesha kujua  kuitafsiri Katiba na kunukuu vifungu vya sheria ya CAG lakini hakwenda mbali zaidi na kusoma sheria.”

“Sheria nyingine ambazo zinaambatana na maagizo hayo ya kikatiba na kisheria katika kufanya tafsiri ya siku ambazo zimeandikwa katika katiba na sheria zinazohusika na uwasilishwaji wa ripoti ya CAG na hasa sheria ya tafsiri za sheria na hivyo kuonyesha wazi kuwa Serikali haitaki kuwajibika ama haijawajibika.”

Mhagama aliomba mwongozo wa kiti kwamba linapotokea jambo kama hilo kiti kinapaswa kuwa tayari kumtafsiria Mnyika tafsiri na sheria hizo zote ili asiendelee kulipotosha Bunge na kuiacha Serikali iendelee kujipanga katika utekelezaji wa jambo hilo.

Katika majibu yake Chenge amesema, “Mnyika tunaongozwa na orodha ya shughuli za Bunge. Katiba kama ulivyoisoma lazima pia usome na sheria ya tafsiri, kwa sababu halikutokea bungeni, hakuna kitu kama hicho, hati zilizowasilishwa ni hizo. Nakusihi kasome sheria ya tafsiri inayoeleza siku na naamini Serikali haijaenda nje ya tafsiri.”