UKATILI: Mtoto achomwa sindano ya sumu

Unguja. Watu wawili wasiojulikana, mmoja akiwa amefunika uso kwa vazi maalumu (ninja) wanadaiwa kumchoma sindano yenye sumu mtoto wa miaka minne (jina linahifadhiwa)katika shehia ya Miti Ulaya mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Tukio la kuchomwa sindano mtoto huyo wa kiume lilitokea juzi majira ya jioni wakati akiwa anacheza na wenzake.

Akisimulia tukio hilo, dada wa mtoto huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema wakati mtoto huyo akicheza na wenzake ghafla lilitokea gari la rangi nyekundu na kushuka watu wawili mmoja akiwa amevaa kininja na mwingine nguo nyeusi juu na chini.

“Baada ya kuwaona watu hao, watoto wengine walikimbia na kumuacha mwenzao ndipo walipomkamata na kumchoma sindano ya kidole na kisha kukimbia na gari yao kwa mwendo wa kasi na kumuacha mtoto huyo akilia,” alisema.

Akizungumza na Mwananchi, mama mzazi wa mtoto huyo, Maryam Said alisema tukio hilo limeshwatua na hawajui sababu.

“Mtoto alirudi nyumbani analia ndipo tulipogundua anatoka damu katika kidole baada ya kuchomwa sindano,” alisema.

Alisema baada ya kuona hali hiyo walimpeleka hospitali binafsi na kupatiwa dawa na kutakiwa kurudi, lakini walipofika nyumbani hali ya mtoto huyo ikaanza kubadilika.

“Asubuhi siku ya pili baada ya kuona kidole kinazidi kuharibika na kutoa taka tulimmpeleka Hospitali Kuu Mnazi Mmoja ambako tulielezwa kuwa amechomwa sindano yenye sumu na kupatiwa dawa huku akitakiwa asile kabisa vyakula vyenye kemikali,” alisema.

Akizungumza na gazeti hili, mkuu wa kitengo cha uchunguzi Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dk Marijani Msafiri amethibitisha kupokea tukio hilo lakini aliahidi kufuatilia ili kupata taarifa za kina.

Kamanda wa Polisi Mjini Magharibi, Thobias Sedoyeka alipoulizwa alikiri kupokea taarifa za tukio na alikuwa akizifanyia kazi.