Mtoto mwenye kichanga adaiwa kunyanyaswa

Muktasari:

Mwenyekiti wa mtaa anaoishi mtoto huyo ambaye pia ana mtoto amezungumza mambo mbalimbali ikiwamo namna walivyobaini kuwa amejeruhiwa; mtoto mwenyewe amezungumza akiwa hospitali alikolazwa
 

Dodoma. Wananchi jana walipishana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kumuona mtoto anayedaiwa kufanyiwa ukatili na mwajiri wake.

Mapema asubuhi zilianza kusambaa mitandaoni picha za video zikimuonyesha mtoto huyo ziambatana na ujumbe ulioeleza kuwa amejeruhiwa na mwajiriwa wake.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alisema wamemkamata mtuhumiwa Anitha Kimako, lakini yuko nje kwa dhamana wakati upelelezi unaendelea.

Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 15 ambaye naye ana mtoto mchanga wa miezi mitano alifikishwa hospitalini hapo juzi na Mwenyekiti wa Mtaa wa Makongoro jijini hapa, Zena Chiuja akiwa na maumivu makali katika sehemu mbalimbali za mwili wake.

Chiuja alisema kilichowafanya washtukie mtoto huyo kuwa amejeruhiwa ni baada ya kutumwa kununua mkaa na mwajiri wake ambapo majirani walishangaa kuona anashindwa kuinama wala kutembea kwa mwendo waliouzoea.

Mwenyekiti huyo alisema walipomuuliza mtoto huyo kwa nini alikuwa akitembea kwa mwendo wa ‘kujivutavuta’ alikataa kueleza ukweli, lakini majirani walimbana na kutishia kumpiga ndipo alipowaambia kuwa amekuwa akipigwa na mwajiri wake kwa kuchelewa kumchemshia maji ya kuoga.

“Alimtaja mwajiri wake ambaye hata mimi namfahamu mwalimu huyo ndipo nikabeba jukumu la kumpeleka polisi huyu binti,” alisema. Chiuja alisema baada ya maelezo walibaini kuwa mtoto huyo ana mtoto mchanga.

Mtoto, daktari wazungumza

Akizungumza hospitalini hapo, mtoto huyo alisema amekuwa akiishi na mwalimu huyo kwa mwaka mmoja na nusu sasa tangu alipomchukua kijijini kwao Kigwe wilayani Bahi mkoani Dodoma.

“Nilipatia ujauzito nikiwa hapo (kwa mwalimu) na aliyenipa ni (anamtaja) lakini toka nimezaa huyu mtoto wangu amekuwa akinipiga,” alisema mtoto huyo.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Ernest Ibenzi alisema alimpokea mtoto huyo akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake, lakini mtoto wake amegundulika kuwa na utapiamlo.

Dk Ibenzi alisema kwa sasa watoto hao ambao ni mama na mwanaye wako katika wodi ya watoto wenye utapiamlo, lakini hali ya kichanga siyo nzuri, hivyo madaktari wanafanya kila njia kuokoa maisha yake.

Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Dodoma, Fatuma Tawfiq alisema watoto hao wana haki kama ilivyo kwa watoto wengine.

Fatuma alisema binti wa kazi anapaswa kulelewa katika mazingira mazuri ili kutomjengea chuki kwani akipandikiziwa hali hiyo anaweza kufanya jambo lolote baya kwa familia na hivyo kusababisha madhara makubwa.

Mkazi wa Dodoma, Elikana Emmanuel aliwataka wazazi na walezi kuzingatia malezi bora kwa watoto hata kama hawakuzaa ili kuwajengea utu ndani ya jamii.

“Mtoto akilelewa vibaya anaweza kugeuka na kuwa mtu wa ajabu sana akishakua, ni wajibu wa wazazi kuwalea vizuri,” alisema.