Muslimu atua Songwe kuchunguza ajali iliyoua 19

Muktasari:

  • Kamanda wa polisi kikosi cha usalama barabarani, Fortunatus Muslimu amewasili mkoani Songwe kuchunguza ajali iliyoua 19 na tayari ameanzia hospitali ya mkoa kuwapa pole wafiwa.

Mbozi. Baada ya juzi kutokea ajali mkoani Songwe na kusababisha vifo vya watu 19, kamanda wa polisi kikosi cha usalama barabarani, Fortunatus Muslimu amewasili mkoani humo kuchunguza ajali hiyo.

Leo Jumamosi Februari 23, 2019, kamanda Silima alikuwa katika hospitali ya mkoa wa Songwe akiwapa pole baadhi ya waombolezaji waliokuwa wakichukua miili ya ndugu zao.

“Tutaungana na wenzetu mamlaka zinazojihusisha na usalama barabarani ili kufikia muafaka na suluhisho la ajali za mara kwa mara,” amesema Muslimu.

Rouben Msinga amesema kitendo cha kamanda huyo kufika kwa haraka na hatua ya Serikali kutoa majeneza na usafiri vimewatia moyo kuwa Serikali inawajali.

Ajali hiyo imetokea usiku wa Februari 21, 2019 katika mteremko wa mlima Senjele baada ya lori lililokuwa likitokea Tunduma kuelekea Mbeya mjini kuligonga basi la abiria kwa nyuma.

Basi hilo baada ya kugongwa liliminywa katikati baada ya kuligonga lori jingine lililokuwa mbele yake.

Watu 18 katika basi hilo wote wamefariki dunia pamoja na  dereva wa lori lililogonga basi la abiria.