Mwakyembe asifu wingi vyombo vya habari, akosolewa

Dodoma. Serikali imesema Tanzania ina vyombo vingi vya habari kulinganisha na nchi nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki, lakini wapinzani wamekosoa takwimu hizo wakisema uhuru wa habari unazidi kudorora.

waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema hayo jana wakati akisoma hotuba ya makadirio na matumizi ya mwaka 2019/20, akiomba Bunge lipitishe Sh30.8 bilioni kwa ajili ya wizara hiyo.

Waziri Mwakyembe pia alisema mchakato wa kusajili vyombo vya habari Tanzania hauna matatizo, akijaribu kuthibitisha kuwa uhuru wa habari nchini ni mkubwa.

Alisema katika miezi michache iliyopita, Serikali ilisajili magazeti mapya saba na kufanya idadi kufikia 216, hadi kufikia Machi 2019.

Hali kadhalika, vituo vipya sita vya televisheni na 15 vya redio vilisajiliwa katika miezi michache iliyopita na kufanya idadi ya vituo vya televisheni kufikia 36 na vya redio kufikia 163.

“Zaidi ya hapo, taasisi 72 zinazotoa habari katika mitandao zilisajiliwa na kufanya idadi yake kufikia 274,” alisema wakati akiorodhesha shughuli kadhaa ambazo wizara yake imezifanya kukuza sekta ya habari.

Waziri Mwakyembe pia alitaarifu kuwa ameshapokea mapendekezo ya wajumbe wa Baraza la Habari ambalo linatarajiwa kuanza kazi mwakani, ikiwa ni utekelezasji wa matakwa ya Sheria ya Huduma ya Habari.

Wizara hiyo, ambayo pia inahusika na utamaduni, sanaa na michezo, imepanga kuchapisha na kusambaza kitabu cha maadili kitakachotumika kutoa miongozo ya maadili ya “kufanya utafiti wa lugha ambazo ziko hatarini kutoweka na kuzungumzwa na jamii kama Segeju, Vidunda, Zaramo na Burunge.

Kuhusu sanaa, Mwakyembe alisema Bodi ya filamu itaendelea na kazi ya kutunga sera ya sanaa hiyo, kupitia pamoja na kuchambua na kuendesha operesheni 36 dhidi ya kazi za filamu zinazoingia sokoni kinyume cha utaratibu.

Kuhusu michezo, Waziri Mwakyembe alisema wizara yake ilisajili vyama 10 vya michezo, klabu 80, vituo vitano na wakuzaji wa michezo 15. Pia inaratibu ushiriki wa timu za Taifa katika mashindano ya kimataifa kama All Africa Games na Olimpiki.

Pia Dk Mwakyembe alisema katika mwaka wa bajeti 2019/2020 itatengeneza mfumo wa kuhifadhi kumbukumbu za vitambulisho na leseni zilizotolewa.

‘Magazeti mengi si hoja’

Pamoja na shughuli hizo nyingi za wizara, wabunge, hasa wa upinzani waliangazia zaidi suala la uhuru wa habari.

Mbunge wa viti maalum (Chadema), Devotha Minja alisema ongezeko hilo la vyombo vya habari si hoja kwa kuwa vinabanwa na kufungiwa.

“Hoja si kuwa na vyombo vingi vya habari. Hoja ni vinafanya kazi kwa uhuru? Au ndio zile ambazo waziri akiamka asubuhi anafungia kwa sababu hayajaandika habari fulani,” alisema Devotha.

“(Ofisi ya) Habari Maelezo hivi sasa imegeuka kitanzi kwa wanahabari. Ukienda katika vyumba vya habari utakuta fomu wameandikiwa na Maelezo wakitakiwa kujieleza kwanini wasifungiwe.”

Alisema idara hiyo badala ya kuelekeza vyombo vya habari vifanye nini, imegeuka na kuyafungia magazeti yanayoandika habari nzuri ambazo haziipendezi Serikali, huku akihoji sababu za habari kukosewa lakini kinafungiwa chombo cha habari badala ya kushughulika na mwandishi husika.

“Mkurugenzi wa maelezo juzi tu ameyataka magazeti yaende kujieleza kwa kuandika habari za kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo aliyeichambua taarifa ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali). Vyombo hivi vilikuwa na haki ya kuhabarisha habari hili lakini vimetakiwa kwenda kujieleza,” alisema Khatib.

Khatib pia alisema kuna magazeti yanaandika habari za kuwadhalilisha watu, lakini hayachukuliwi hatua yoyote,

“Kwanini hawaitwi wapo nyuma ya nani? Wapo wengine wakitoa maoni kidogo tu wanashtakiwa.”

“Inasaidia nini kuwa na magazeti mengi lakini waziri anaweza kuamka tu asubuhi akayafuta?” alihoji Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema) huku akipongeza badhi ya taasisi za habari na sheria kwa kushinda kesi ya kupinga vifungu vya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.