Mwakyembe awashangaa wanaohoji kutoweka Azory Gwanda

Muktasari:

  • Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ametoa kauli hiyo leo Jumanne Aprili 23, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti ya wizara mwaka wa fedha 2019/2020.

Dodoma. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ameshangazwa na wabunge wanaohoji kutoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa mwandishi wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) mkoani Pwani, Azory Gwanda.

Amesema mwandishi huyo aliyetekwa na watu wasiojulikana Novemba 21, 2017 amepotea katika mazingira ambayo Watanzania wengi wamepotea katika eneo hilo (Kibiti).

Waziri huyo ametoa kauli hiyo leo Jumanne Aprili 23, bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo mwaka wa fedha 2019/2020.

“Tunaongelea kesi ambayo ni dhaifu sana, mwandishi huyu amepotea eneo ambalo mamia ya Watanzania wengine wamepotea, hawauliziwi hao ila mmoja huyo ndio dhahabu.”

“Halafu inaulizwa Serikali ambayo imeshughulikiwa kiasi kikubwa na maofisa wa Serikali wengi wamekufa pale, najua mnawalisha Wazungu na wafadhili matango pori (uongo), hatujakosa chochote acha tushushwe madaraja, sisi tunaheshimu uhuru wetu kwanza,” amesema.

Kwa mujibu wa mke wa Azory, Anna Pinoni (35), siku hiyo asubuhi watu wanne wakiwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe walifika katikati ya mji wa Kibiti sehemu ambayo Azory hupatikana mara kwa mara na kumchukua.

Watu hao walimpeleka hadi shambani ambako mkewe alikuwa akilima na akamuaga kuwa anaenda kazini lakini hajarudi hadi leo.