VIDEO: kitendawili cha azory Gwanda chatimiza mwaka mmoja

Muktasari:

Mwandishi huyo wa kampuni ya Mwananchi alitoweka baada ya kuchukuliwa na watu ambao hadi leo hawajajulikana na waliokuwa na gari nyeupe.


Leo umetimia mwaka mmoja tangu mwandishi wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) mkoani Pwani, Azory Gwanda atekwe na watu wasiojulikana Novemba 21, 2017.

Azory anatimiza mwaka mmoja huku nyuma akiwa ameacha alama kubwa; kwanza katika familia yake ambako anazidi kukumbukwa na ndani ya tasnia ya habari aliyokuwa akiifanyia kazi kabla ya kukumbwa na mkasa huo.

Kwa mujibu wa mkewe, Anna Pinoni (35), siku hiyo asubuhi watu wanne wakiwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe, walifika katikati ya mji wa Kibiti, sehemu ambayo Azory hupatikana mara kwa mara, na kumchukua.

Watu hao walimpeleka hadi shambani ambako mkewe alikuwa akilima na akamuaga kuwa anaenda kazini, lakini hajarudi hadi leo.

Akizungumza mwaka mmoja tangu kutoweka kwa mpendwa wake, Anna Pinoni hakusita kuonyesha hisia zake akisema bado anampenda na atamkumbuka daima.

Anasema kuishi bila mwenza wake umekuwa mtihani usioelezeka, hasa kwa vile hadi sasa hajui kama angali hai.

“Mume wangu alikuwa akiipenda sana kazi ya uandishi wa habari na tangu tunafunga ndoa aliniambia jinsi anavyoipenda kazi hii,” alisema Pinoni katika mahojiano na Mwananchi.

“Na mimi nilimwambia kwa kuwa alikuwa mwongeaji sana hii kazi itamfaa.

“Naamini kutoweka kwake kumechangiwa na kazi alizokuwa akizifanya licha ya kwamba alikuwa akitoa habari za kweli tena alizozifanyia uchunguzi mkubwa. Alikuwa akihoji wahusika wote, hakutoa taarifa bila kuikamilisha. Yaani akitangaza habari basi ilikuwa habari haswa wala hakufanya mchezo.”

Mke huyo hajavunjika moyo wala kukata tamaa kumsaka mumewe na anaiomba Serikali iendelee kusaidia kupatikana kwake

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi mtendaji wa MCL, Francis Nanai kuelezea tukio la mwandishi huyo, inasema baada ya kumchukua, gari hilo lilielekea

shambani kwake saa 4:00 asubuhi na kumkuta mkewe.

Alieleza kuwa Azory, aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma, alimuita mkewe kutokea upande huo wa gari na kumuuliza alikoweka ufunguo wa nyumba yao.

Nanai anasema mkewe alilisogelea gari na kuzungumza naye kutokea dirishani na kumweleza alipouficha ufunguo, huku Azory akimwambia amepata safari ya dharura na kama asingerudi siku hiyo ya Novemba 21 basi angerudi siku inayofuata.

Anasema gari hilo liliondoka na kwenda nyumbani ambako mkewe alieleza kuwa aliporudi alikuta kuna upekuzi umefanyika kwa sababu alikuta vitu viko shaghalabaghala.

Kwa ujumla taarifa za kutoweka kwa Azory zilitangazwa kwa mara ya kwanza Desemba 7, 2017 katika mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali wa habari. Mkutano huo ulifanyika ofisi za makao makuu ya MCL zilizopo Tabata Relini, Dar es Salaam.

Baadaye, MCL iliendesha kampeni ya kumtangaza Azory kwenye kurasa za mbele za magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti na mitandao yake kwa kipindi cha siku 100. Licha ya juhudi zote hizo, hadi Machi 1, 2018 wakati zilipotimia siku 100 hakuna taarifa iliyotolewa na chombo chochote kuhusu mahali Azory alipo.

Leo, wakati ukitimia mwaka mmoja, familia yake imeongezeka kutoka mtoto mmoja hadi wawili kwa kuwa Azory alitoweka wakati mkewe akiwa na ujauzito. toto wao Gladness aliyezaliwa Februari, hamjui baba.

Familia yake inasema bado inaendelea kumkumbuka wakati wote na haijakata tamaa kuomba mamlaka za dola kusaidia kupatikana kwake.

Katika tasnia ya habari, Azory anamaliza mwaka mmoja huku akiwa ameacha alama iliyochora mstari kuhusu usalama wa waandishi wa habari Tanzania. Mazingira ya kutoweka kwake, yaliusukuma Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kumtunuku tuzo ijulikanayo kama Daudi Mwangosi.

Tuzo hiyo iliyotolewa Septemba, inathamini kazi yake kutokana na mchango wake wa kuripoti bila woga matukio mbalimbali, yakiwemo ya mauji yaliyotikiisa nchi ya viongozi katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji.

Tuzo hiyo ni kumbukumbu ya kifo cha Daudi Mwangosi, aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten na mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari ya Mkoa wa Iringa. Mwangosi aliuwa na polisi wakati akitekeleza majukumu yake.

Wakati akimtangaza mshindi wa tuzo hiyo, mwenyekiti wa jopo la majaji wa tuzo hiyo, Ndimara Tegambwage alisema Azory alithubutu kuripoti matukio hayo bila woga, lakini katika mazingira ya kutatanisha alitekwa na kupelekwa kusikojulikana na hadi sasa haijulikani kama yupo hai au amefariki dunia.

Habari za kutoweka kwa Azory ziliendelea kutawala vyombo vya habari huku matamko ya aina mbalimbali yakikemea kitendo hicho na kukielezea kuwa ni cha uvunjaji wa haki za binadamu kinachostahili kudhibitiwa mapema.

Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania ya mwaka 2017 iliyotolewa Aprili 24, ilisema tukio la kupotea kwa Azory linaichafua Tanzania.

Akiwasilisha ripoti hiyo, mtafiti wa haki za binadamu, Fundikira Wazambi alisema kutoweka kwa mwandishi huyo kumesababisha taharuki kwa wanahabari.

Wakitambua mazingira magumu wanayokabiliana nayo, waandishi wa habari walijumuika pamoja wakati wa sherehe za kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Habari Duniani Mei 3, 2018 na kutoa tamko la pamoja kulaani kitendo hicho.

Mwenyekiti wa Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (Misa- Tan), Salome Kitomari alisema ni muhimu hatua zichukuliwe kukabiliana na hali iliyopo.

Kitomari alisema takwimu za taasisi kama ya waandishi wasio na mipaka na kamati ya kulinda waandishi wa habari zinaonyesha kushuka kwa viwango vya uhuru wa habari na kujieleza Tanzania.

“Lakini pia matukio ya utekwaji nyara na viwango vya unyanyasaji wa wanahabari duniani vimeongezeka sana,” alisema.

“Leo ni siku ya 163 (Mei 3, 2018) tangu kupotea kwa mwandishi wa habari wa Mwananchi, hakuna hata fununu tu yupo wapi, yupo hai au la ni jambo ambalo linaitia doa nchi yetu.”

Soma Zaidi: