Ndalichako kugawa tuzo shule zilizoongeza ufaulu

Muktasari:

  • Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako atagawa tuzo kwa wanafunzi na shule 40 ambazo zilifanya vizuri katika mitihani ya kitaifa mwaka jana  na zile zilizoongeza ufaulu .

Dodoma. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako atatoa tuzo kwa shule na wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya kuhitimu shule za msingi na sekondari mwaka 2018.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara hiyo Sylvia Lupembe leo Jumatano Juni 12 2019, wakati akielezea kuhusu maadhimisho ya siku ya Elimu kitaifa yatakayofanyika Ijumaa Juni 14 katika Shule ya Wasichana ya Msalato jijini Dodoma.

“Lengo ni kuendelea kuthamini na kutambua juhudi za wanafunzi katika masomo yao. Lakini vilevile kutambua juhudi za shule kwa maana ya jumuiya mbalimbali zilizofanya vizuri,” amesema.

Amesema wanafunzi 29 bora kwa shule za msingi, Sekondari kidato cha nne na sita watapokea tuzo na kwamba shule 40 zitapatiwa tuzo.

Amefafanua kuwa shule 20 zitakuwa zilizofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa na zinazosalia zitapewa tuzo kwa kuongeza ufaulu.