Ndugai: Bunge halifanyi kazi na Profesa Assad, si ofisi ya CAG

Muktasari:

SpikaJob Ndugai amesema Bunge linafanya kazi na ofisi ya CAG na si Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema Bunge lilitangaza kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na si ofisi yake.

Ndugai ametoa kauli hiyo leo mchana Alhamisi Aprili 4, 2019 baada ya kuwatambulisha wageni walioalikwa bungeni, akiweka sawa hali ya sintofahamu iliyoibuka baada ya Bunge kutangaza kutofanya kazi na Profesa Assad.

“Hakuna wakati wowote ambao Bunge limekataa kufanya kazi na taasisi ambayo ni ofisi ya CAG. Bunge hili limekataa kufanya kazi na mtu anayeitwa Profesa Assad basi. Tusiripoti tofauti tukauchonganisha umma na kuuchanganya,” amesema Ndugai.

Aprili 2, 2019 Bunge lilipitisha azimio la kutofanya kazi na Profesa Assad kwa sababu ya kauli yake aliyoitoa wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuwa Bunge ni dhaifu.