Ndugai: Suala la Bunge na CAG ni la muda

Muktasari:

Taasisi hizo mbili zimeingia katika mgogoro baada ya Spika Job Ndugai kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad kufika mbele ya kamati kujieleza kuhusu kauli yake kuwa chombo hicho cha kutunga sheria ni dhaifu katika utekelezaji wa majukumu yake, ikiwa ni pamoja na kufuatilia kasoro zinazobainishwa kwenye ripoti za ukaguzi.

Dar/Dodoma. Spika Job Ndugai amesema mzozo kati ya Bunge na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad ni wa muda, “Utamalizika muda wowote ila siwezi kusema ni keshokutwa au nini.”

Ndugai alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na Mwananchi kuhusu uamuzi wa Bunge kutofanya kazi na ofisi ya CAG sambamba na kuwapeleka wajumbe wa kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac) katika kamati nyingine. Kamati hizo zinazoongozwa na upinzani ndizo zinahusika na uchambuzi wa ripoti ya ukaguzi ya CAG.

Wakati Ndugai akieleza hayo, mzozo huo umechukua sura mpya baada ya kesi ya kupinga uamuzi wa Spika huyo kumuita CAG katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Januari 21 kubaki njia panda baada ya jana kushindwa kusajiliwa.

Hayo yakitokea, wanasheria nao wametahadharisha kuhusu mzozo huo, wakisema utaipeleka nchi pabaya huku wabunge wa upinzani wakitaja mambo manne waliyodai kuwa chanzo cha Spika kutotaka Bunge kushirikiana na CAG, na kwamba iwapo hatobadili uamuzi wake huo, watapeleka taarifa ya kutokuwa na imani naye.

Mzozo kati ya Ndugai na CAG ulianza baada ya Profesa Assad wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kusema kushindwa kutekelezwa kwa ripoti anazowasilisha bungeni huenda kunatokana na udhaifu wa chombo hicho kauli ambayo Ndugai alisema ni ya kudhalilisha Bunge na kumtaka kufika mbele ya kamati hiyo kuhojiwa.

Jana, Ndugai alisema, “Huwezi kuwa na Bunge ambalo halina CAG hawezekani, ila ni kwa muda tu. Kwa sasa siwezi kusema mpaka keshokutwa au nini.”

Alisema kamati ya maadili ni kama mahakama ndogo, “Unapokuwa unashtakiana na mtu haiwezekani mshtakiwa wako mnakaa chemba tena wakati inatakiwa tarehe 21 atokee katika hicho chombo (kamati).”

“Hamuwezi kuendelea kuwa na mahusiano ya kawaida na mtu yule. Wewe ni jaji katika mahakama kuna mtuhumiwa ameonekana mnakaakaa huko... inaendaga hivyo?”

Alisema kutokana na hali ilivyo sasa, hawawezi kuendeleza uhusiano wa kawaida na CAG mpaka mzozo huo utakapomalizika.

“Naamini linakwisha haraka sana, likiisha mambo mengine yataendelea. Hatuwezi kujifanya hakuna kilichotokea wakati tuna tatizo ambalo kila mtu analijua.”

Ndugai pia alijibu hoja za wapinzani walizozitoa jana mjini Dodoma kuwa uamuzi wake haukushirikisha Kamati ya Uongozi ya Bunge na kwamba una lenga kufisha mjadala wa Sh1.5 trilioni ambazo matumizi yake hayakuonekana katika ripoti ya CAG, kuficha ukweli wa fedha za miradi mikubwa ya ununuzi wa ndege na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na kutaka kuyumbisha msimamo wa Profesa Assad, madai ambayo yalitolewa na wabunge wa upinzani wakiongozwa na John Mnyika (Kibamba).

Akijibu hoja hizo, Ndugai alisema, “Upinzani wa Tanzania shida yake ni upotoshaji mwanzo mwisho. Ishu ilivyoanza hadi sasa inajulikana na tunachokilalamikia mnakijua. Tazama katika vitabu vya CAG kama kuna hoja ya Sh1.5 trilioni. Hiyo haijawahi kuwa hoja.”

“Hakuna kinachofichwa katika kamati na ndio maana wenyeviti wake (PAC na Laac) wanatokea upinzani. Kama tungekuwa na nia ya kuficha si kamati zingeongozwa na CCM.? Hivyo ni vitu vya kutunga na muda utaeleza kama tulikuwa na lengo la kuficha au kutokuficha. Suala la Sh1.5 trilioni lilitolewa maelezo na Serikali mwaka jana, si waichukue hiyo waichambue maana ina matumizi yote.

Kesi ilivyokuwa

Wabunge watano wa vyama vitatu vya upinzani, wakiongozwa na Zitto Kabwe (Kigoma Mjini - ACT- Wazalendo), jana walikwama kusajili kesi yao baada ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kukataa kwa madai kwamba ina kasoro za kisheria.

Kutokana na uamuzi huo, Zitto na wakili wao, Fatma Karume waliwasilisha malalamiko kwa Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma ambaye baada ya kuyasikiliza, alimwandikia barua Jaji Kiongozi akimwelekeza ashughulikie suala hilo.

Wabunge wengine katika kesi hiyo ni Saed Kubenea (Ubungo-Chadema), Salome Makamba (Viti Maalumu Chadema), Hamidu Bobali (Mchinga -CUF), na Anthony Komu (Moshi Vijijini - Chadema) ambao wote walikuwa wanaiomba Mahakama hiyo itoe tafsiri ya kinga ya CAG iliyopo kikatiba na pia kutoa tafsiri ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge katika kushtaki watu wanaosemekana kudharau Bunge.

Katika barua yake ya kutokuisajili kesi hiyo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu aliyejitambulisha kwa jina la S.S. Sarwatti alidai kuwa hawezi kuipokea kwa kuwa wadaiwa wanne katika shauri hilo hawakuambatanisha hati zao za viapo katika hati ya maombi, kwani kuna kiapo cha Zitto pekee.

Pia hati ya maombi hayo haina hati ya wito wa Spika kwa CAG na au hati ya kiapo ya CAG haikuambatanishwa.

Wakili Karume alisema hata baada ya kufanya marekebisho kwa kuwaondoa wadai wengine ambao hawakuwa na viapo vyao katika kesi hiyo, bado naibu msajili alisisitiza kutokuwepo kwa wito wa Spika kwa CAG au kiapo chake.

Kauli za wanasheria

Alipoulizwa maoni yake kuhusu sakata hilo, Wakili Dk Onesmo Kyauke alisema si sahihi Bunge kukataa kufanya kazi na ofisi ya CAG kwa kuwa ndiyo inafanya ukaguzi na kupeleka sehemu zenye matatizo bungeni ambako kamati za Bunge hufuatilia.”

Mhadhiri wa Sheria wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Jesse James alisema, “Ni jambo la kusikitisha kwasababu linafuga mgogoro mkubwa.

Lakini CAG mstaafu Ludovick Utouh alisema anaamini itakapofika Januari 21, Bunge litapatana Ofisi ya CAG na mambo yatakwenda vizuri.