Ndugai: Tumempa CAG barua ya wito

Muktasari:

Baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kusema Bunge ni dhaifu, Spika Job Ndugai alizungumza na wanahabari na kueleza jinsi alivyochukizwa na kauli hiyo, amesema tayari ofisi yake imeshamuandikia barua ya wito ikimtaka kufika mbele ya Kamati ya Maadili, Kinga na Haki ya Bunge ili kuhojiwa


Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema ofisi yake tayari imeshaandika barua ya wito kwenda ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikimtaka kufika mbele ya Kamati ya Maadili, Kinga na Haki ya Bunge ili kuhojiwa.

Hatua hiyo imekuja siku tatu baada ya Spika Ndugai kumtaka CAG, Profesa Mussa Assad kufika mbele ya kamati hiyo kujieleza kuhusu kauli yake kuwa chombo hicho cha kutunga sheria hakitekelezi ipasavyo majukumu yake ya kuisimamia Serikali.

Profesa Assad, ambaye ametakiwa kufika mbele ya kamati hiyo Januari 21, alitoa kauli hiyo alipohojiwa na idhaa ya Kiswahili ya kiutuo cha televisheni cha Umoja wa Mataifa (UN), wakati alipokuwa jijini New York, Marekani kuhudhuria mkutano wa jopo la wakaguzi wa njei.

Mbali na CAG, mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee naye ameitwa mbele ya kamati hiyo Januari 22 kwa madai ya kutoa kauli iliyounga mkono kilichosemwa na Profesa Assad.

“Tayari tumeshamwandika barua yaani summons (hati ya wito), maana wito wetu unaenda kama wa kimahakama vile,” alisema Ndugai kwa njia ya simu jana, muda mfupi baada ya kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa mawaziri wawili na wateule wengine wa Rais Ikulu jijini Dar es Salaam.

Wakati Ndugai akisema hayo, katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif amemtaka Ndugai kumuomba radhi Profesa Assad akisema kilichofanywa na CAG ni kutimiza wajibu wake na si kulidhalilisha Bunge.

“Unafikiri ripoti za aina hii (za ukaguzi za CAG) hufanyika siku moja au mbili, hapana. Hutumia zaidi akili na muda, ndio maana inaumiza sana mwisho wa siku huoni hatima ya ripoti, unadhani Profesa Mussa atasemaje kama sio udhaifu wa Bunge,” alisema Maalim Seif alipozungumza na Mwananchi akiwa Pemba.

Juzi, mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Kinga na Haki ya Bunge, Emmanuel Mwakasaka aliliambia gazeti hili kuwa endapo CAG ataona ni vigumu kujieleza mwenyewe mbele ya kamati, anaweza kwenda na mwanasheria wake.

Ndugai amekuwa akiwaita mbele ya kamati hiyo watu ambao wamekuwa wakitoa maoni yao wakidai kuwa Bunge limekuwa dhaifu.