Ngoma nzito mgogoro wa kugombea maiti Moshi

Muktasari:

  • Familia yamkana mwanamume anayetaka kumzika mkewe, yahoji cheti cha ndoa

Moshi. Familia ya mfanyabiashara Fatuma Kileo ambaye mumewe Zuberi Shango anataka apewe haki ya kumzika, imemkana mwanamume huyo ikidai ndoa anayodai kufunga na ndugu yao ni bandia.

Pia, familia hiyo kupitia kwa mujibu maombi wa kwanza, Ausen Nkya imedai cheti cha ndoa alichonacho Shango ni cha bandia na kipindi chote cha uhai wake Fatuma hakuwahi kubadili dini kutoka ukristo na kuwa mwislamu.

Hayo yamo katika hati ya kiapo kinzani ya Ausen ambaye ni mmoja wa wajibu maombi, kilichowasilishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi jana na Wakili Godwin Sandi.

Mbali na kuwasilisha majibu hayo, lakini wajibu maombi hao wanaotetewa na Wakili Sandi, pia wamewasilisha pingamizi la awali wakidai kesi imefunguliwa kimakosa na kwa sheria isiyo sahihi.

Shango amewashtaki wanafamilia wawili ambao ni Ausen Nkya kama mshtakiwa wa kwanza na Lodriki Kileo akiwa ni wa pili katika kesi hiyo inayovuta hisia za wananchi wengi.

Kwa mujibu wa maombi namba 24 ya 2018 yaliyowasilishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi juzi, mume huyo anadai alifunga ndoa na Fatuma, Julai 20, 2005 huko Tunduma mkoani Mbeya (sasa mkoa wa Songwe).

Shango anadai walifunga ndoa ya Kiislamu na hati ya ndoa ina namba 6306, iliyotolewa na Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Mbeya na ilisimamiwa na Sheikh Idrisa Adeny.

“Kabla ya kufunga ndoa hii, mke wangu alikuwa akijulikana kwa jina la Betty Assery Kileo, jina ambalo alipewa na wazazi wake na ndilo linaloonekana kwenye cheti chake cha kuzaliwa,” alidai.

Katika hati ya madai, Shango alidai wajibu maombi wanamzuia asimzike mkewe kwa hofu kuwa kama atamzika kwa imani ya Kiislamu atakuwa na haki ya kurithi mali za marehemu.

Fatuma alikuwa akifanya biashara ya kusafirisha mazao kwenda nchi jirani na anadaiwa pamoja na mali zingine anamiliki nyumba yenye thamani ya Sh80 milioni katika mji mdogo wa Himo.

“Sina nia yoyote ya kuchukua au kurithi mali za marehemu, lakini nitaziacha mali zote kwa watoto wa marehemu. Ninachotaka mimi ni kumzika mke wangu,” alidai.

Fatuma, ambaye alikuwa mfanyabiashara maarufu katika mji mdogo wa Himo wilayani Moshi, alikuwa anamiliki biashara na nyumba ya kuishi inayokadiriwa kuwa na thamani ya Sh80 milioni.

Sababu za kumkana mume

Katika hati ya kiapo kinzani walichokiwasilisha mahakamani jana, wajibu maombi wawili; Nkya na Kileo wanasisitiza kuwa Fatuma hakuwahi kuolewa wala hakufia Hospitali ya Kilema.

Badala yake, wajibu maombi hao ambao ni ndugu wa mwanamke huyo wanadai alifia nyumbani kwake Himo na mwili wake ulipelekwa Hospitali ya Kilema na ndugu kwa ajili ya kuuhifadhi.

Nkya, ambaye ndiye aliyesaini kiapo hicho alidai hakuna mwana familia wa Fatuma aliyewahi kushiriki tukio la kufungwa kwa ndoa inayotajwa na Shango wala hawamfahamu mlalamikaji.

Katika kiapo hicho, Ausen ameenda mbali na kueleza kuwa hata watoto watatu wa mwanamke huyo ambao alikuwa akiishi nao katika nyumba yake iliyopo Himo hawakuifahamu ndoa hiyo.

“Fatuma hakuishi na muombaji (Shango) kabisa. Aliishi na watoto wake watatu Alex Mollel, Faustin Benard na Getrude Sylvester na hajawahi kuishi maisha ya Kiislamu,” ameeleza Ausen.

“Badala yake alikuwa Mkristo kama walivyo watoto wake na wakati wote wa maisha yake walikuwa wakienda kanisani kusali pamoja na watoto wake.”

Mujibu maombi huyo amedai hakuwa peke yake wala na mujibu maombi wa pili (Lodriki Kileo), katika kumzuia muombaji (Shango), kuchukua mwili na kumzika Fatuma kwa imani ya dini ya Kiislamu.

Badala yake, Ausen alidai wana familia zaidi ya 100 ndiyo walioamua kumzika na yeye binafsi hana sauti katika masuala yanayohusu familia yao kwa vile si kiongozi wao.

Kesi hiyo iliyowasilishwa chini ya hati ya dharura imepangwa kusikilizwa leo saa 6:00 mchana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Moshi, Bernadetha Maziku.