DPP awafutia mashtaka watuhumiwa watatu wa mauaji Geita

Muktasari:

  • Watuhumiwa hao walikuwa wanashtakiwa kwa mauaji wakidaiwa kumuua kwa kukusudia Hamis Sabi, mkazi wa Nyakafuru, wilayani Mbogwe wakimtuhumu kuiba mbuzi.

Geita. Mahakama Kuu Kanda ya Geita imewaachia huru washtakiwa watatu, Malale Magaka, James Malimi na Kijinga Lugata waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya mtu waliyemtuhumu kuiba mbuzi.

Washtakiwa hao wameachiwa huku baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuiondoa mahakamani akisema hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao.

Watuhumiwa hao wanashtakiwa kwa kumuua kwa kukusudia Hamis Sabi, mkazi wa Nyakafuru, wilayani Mbogwe mkoani Geita wakimtuhumu kwa wizi wa mbuzi.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, watuhumiwa hao walidaiwa kutenda kosa hilo Septemba 16, 2022 huko Nyakafuru wilayani Mbogwe mkoani Geitata, kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya adhabu, sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kesi hiyo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka leo kuanzia leo Jumatatu Aprili 29, 2024, mbele ya Jaji Griffin Mwakapeje.

Hata hivyo, baada ya kuitwa, Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali Verena Mathias ameieleza Mahakama kuwa DPP hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Mkurugenzi wa Mashtaka, hana nia ya kuwashtaki washtakiwa wa kwanza hadi watatu kwa kosa la mauji na hivyo tunaomba kuondoa mashtaka dhidi ya washtakiwa,” amesema Mathias.

Kutokana na taarifa hiyo, Jaji Mwakapeje ametoa amri ya kuwaachilia huru washtakiwa hao wote.

Hata hivyo, Jaji Mwakapeje amewaeleza washtakiwa hao kuwa kuachiwa kwao chini ya kifungu cha 91, haina maana kuwa hawatakamatwa tena endapo DPP ataona sababu za kufanya hivyo.

Washtakiwa hao walikuwa wanatetewa na Vianey Mbuya (wa mshtakiwa wa kwanza) na Beatrice Amos aliyekuwa akiwatetea washtakiwa wa pili na wa tatu.