Ni 2019, hivi Hamisa bado ana miaka 24?

Saturday January 5 2019

 

Morogoro mjini jioni. Jua likianza kupoteza makali yake kwa kufifia upande wa Magharibi. Nipo hotelini nikitokea Iringa, sikutaka kupitiliza Dar. Nilipania kuukaribisha mwaka nikiwa Mji Kasoro Bahari. Wakati mwingine maisha yanahitaji mazingira mapya.

Nautafakari mji wenye ardhi iliyolaza miili ya wanamuziki nguli nchini. Mbaraka Mwinshehe. Salum Abadala na juzi tu udongo mwekundu wa Kihonda uliumeza mwili wa Albert Mangwea. Wote kwa nyakati tofauti walifariki wakiwa wadogo. Moro ina historia na muziki.

Fikra zangu ziliondoka kwa kasi ya kimbunga baada ya ujio wa mhudumu chumbani. Yes ni wa kike... aliyeniletea chakula. Ingawa kilikuwa cha kibwege tu “eti ugali na samaki kitoga” sijui kutoka bwawa la Mindu? Lakini kilionekana bora kutokana na ubora wa mhudumu.

Hakufaa kufanya ile kazi, pia alifaa. Hakufaa kwa faida yake maana hotelini vishawishi ni vingi. Wageni wa kila aina wenye tabia za kipuuzi na za Kiinjilisti anakutana nao. Alifaa kwa faida ya mwenye hoteli maana kitakachofanya nilale tena pale siku nyingine ni yule mrembo.

Ni wale wasichana ambao ukiwa naye unatumia mpaka pesa ya ada za watoto na hujutii. Na unapohangaika kusaka upya pesa huoni kama yeye ndo kikwazo. Kuna warembo unahonga pesa unaona haitoshi unatamani umpe mpaka moyo, mapafu, maini na bandama ziwe zake milele.

Kuna ‘time’ siwalaumu kina marehemu Kanumba, Ray Kigosi na wenzao walipoanza kujaza warembo kwenye filamu bila kujali vipaji. Huyu siyo tu ningempa ‘sini’ acheze, hata malipo kwa ‘Mdosi’ Kariakoo, ningetoa ruhusa kwake akuchukue akatumie atakavyo. “Anafanya nini huku wakati vibweka tu vya kike vinatajirika kwa urembo Dar?” Niliwaza wakati anatoka baada ya kunihudumia. Ndipo nikagundua kuwa pia ana utajiri mkubwa kwenye ncha ya uti wa mgongo. Kavimbaa. Tayari katika ‘phone book’ niliongeza jina lake.

Sipendagi ujinga mimi. Hizi bahati hutokea mara chache kwenye uso wa Dunia hii. Naanzaje kuukaribisha mwaka kwenye mji wa watu kibwege kwa kulala na kujikunyata kama paka kwenye unga? Kesho yake njiani nikirudi Dar uso ulikuwa na nuru ya kuukaribisha mwaka vyema.

2018 ndiyo imeisha hivyo. Hii ni 2019 tukielekea 2020. Sasa wewe dada sijui ‘Sista Duu’ endelea kumsubiri mwanaume mrefu, handsome, aliye na ndinga, msomi, mweupe, mwenye kazi nzuri, au ‘supa staa’ na pesa nyingi utadhani wewe tu ndo mpenda vitu vizuri. Nasema hivi endelea kusubiri.

Madem wa mjini vituko sana, leo ngoja tuwekane sawa. Akigundua mwenzake kamzidi hata wiki moja kiumri ni kosa. Utasikia anamuita Da Nuru, Da Jesca, Da Lisa. Wanapenda utoto kuliko ndoa. Ukisema chagua pesa, ndoa au umri mdogo. 90% watachagua utoto. Hawataki kuzeeka.

Nd’o maana wanasherehekea ‘besidei’ bila kutaja umri. Hata wanaotaja hupunguza miaka utadhani wanataka kusajiliwa Man United. Atakuambia ana miaka 24, na ameanza kutoka kimapenzi na Diamond miaka tisa iliyopita. Ina maana kaanza ngono na miaka 14? Hamisa Mungu anakuona.

Siyo mbaya baadhi ya mastaa tukiwakadiria umri kulingana na walichowahi kukifanya nyuma. Ili tuweze kujua wangapi wanaelekea uzeeni. Maana kila wakifanya ‘besidei’ zao wote wanacheza kwenye miaka 21 mpaka 29. Namba 30 inawakera mastaa wengi sana.

Tunasaidia wanaofanya upuuzi wakijiona watoto. Au kutojipanga kimaisha wakiamini muda bado. Wanaongopa mpaka wanasahau umri sahihi. Wapo wa kitambo hawaongezeki miaka mpaka unajiuliza wenzetu wana mashine za kusimamisha miaka?

Staa mkubwa zaidi wa kike baada ya Amina Chifupa (marehemu) ni Wema Sepetu. Alishiriki na kubeba taji la Miss Tanzania mwaka 2006. Hapo changanya yeye Uwoya, Jokate, Aunt Ezekiel na wenzao. Hiki ni kizazi cha Miss Tanzania kilichovamia Bongo Movie na kuiteka kikatili.

Kuanzia mwaka 2006 mpaka sasa ni miaka 13. Na Miss Tanzania mshiriki anatakiwa awe na miaka kuanzia 18 mpaka 22. Kwa hiyo hapa tuwape wote miaka 19 pale waliposhiriki Miss Tanzania mwaka 2006. Sasa tupige hesabu rahisi sana mpaka sasa wana umri gani?

2006 mpaka sasa ni miaka 13 hivyo ukijumlisha na ile miaka 19 unapata miaka 32. Kwa hiyo umri kwa Wema na wenzake hao washiriki wa Miss Tanzania mpaka sasa ni miaka 32. Inaweza kuzidi zaidi ya hapo ila haitaweza kupungua zaidi ya mwaka mmoja. Huo ndo ukweli.

Kama walikuwa na miaka 17 au 16 wakaongopa kupata uhalali wa kushiriki Umiss. Wanastahili mashitaka wao na Anko Hashim Lundenga wao, changanya na kina Bosco Majaliwa sukumia ndani. Kisha kamata Basata wote fyekelea ndani, kwa kuacha washiriki watoto. Ebo! Malkia wa kaskazini Jack Wolper ‘Gambe’ haeleweki. Kafanya umachinga wa sufuria. Alitoka kimapenzi na King wa Kariakoo akiwa bado siyo staa. Piga hesabu ya kumaliza shule, umachinga na King wa Kariakoo akiwa ‘andagraundi’. Unagundua naye kala chumvi kama yote.

Elizabeth Michael ‘Lulu’ mwaka 2011 aliwahi kufanya ‘besidei’ ya kutimiza miaka 18. Mwaka 2012 alipopata kesi ya kifo cha Steven Kanumba umri wake ukaendelea kuwa miaka 18 tena kama 2011. Huenda matatizo ya yalifanya aseme ukweli au uongo ili kuweka vyema mazingira ya kesi.

Wacha tusimamie miaka 18 ya mwaka 2012 ambayo naamini ndo ukweli. Kale katoto kalifanya ‘besidei’ ya kutimiza miaka 18 mwaka 2011 ili kaanze kuruhusiwa kuingia klabu na kutandika ulabu. 2012 mpaka sasa ni miaka 7. Miaka 18 ongeza miaka 7 ni 25. Lulu ana 25 sasa.

Wako mastaa wengi wasiotaka kuweka wazi umri bila sababu za msingi. Ni kutoelewa faida ya uwazi katika vitu vya msingi kama hivi. Wanaishi na kuongopa utadhani walikuja Bongo kama mizimu. Kwamba hakuna waliosoma nao wala kucheza nao mdako.

Acheni Samatta na kina Msuva wadanganye umri. Kwa sababu mpira ndio ajira yao na ni kazi ya muda mfupi sana. Ukizingatia miili ya Kiafrika haikongoroki ovyo kama wenzetu weupe. Lakini mwigizaji au mwanamuziki unadanganya ili iweje? Hapa ndipo wanashangaza.

Mwigizaji unazeeka na mashabiki. Kadri umri unavyosogea ndivyo unavyozidi kukamata mashabiki kutokana na uhusika wako. Hata wanamuziki pia. Will Smith anazeekea kwenye sanaa. Walioanza kucheza soka yeye akianza kuigiza wako wapi?

Koff Olomide Baba la Baba nusu ya maisha yake ni angani kama mwewe. Sijui mwaka wa 40 huu yuko juu na muziki wake. Anaendelea kutengeneza pesa mpaka uzeeni. Mwanasanaa ni kama ‘mvinyo’ anavyozeeka ndivyo anavyozidi kuwa bora zaidi kisanaa.

Advertisement