Ni Nandy na Ruby, pia tusisahau kuna Fiesta

Saturday July 13 2019

 

Niko ndani ya Mbeya. Mwishoni mwa wiki iliyopita, nimejiegesha kwenye viti virefu. Kiwanja kimoja cha kuondoa ‘stress’ chenye jina la Kinyakyusa hasa. Nasubiri muda ufike niangalie Afcon. Ndo burudani iliyobakia baada ya Pierre kurudi Dar kinyonge na Stars yetu.

Nakunywa maji kama dozi ya dengue. Wahudumu wanapita na kunitazama. Sikuthubutu hata punje wala kujidanganya kuamini kama wanavutiwa na sura yangu. Nina akili zangu timamu. Najua tu walishindwa kuelewa maji yalivyo tofauti na uso wangu. Uso wa ngumu kumeza huu.

Ghafla ukutani kwenye runinga ikaonyesha wimbo wa Nandy. Sikumbuki jina, kila mtu anageuka kuutazama. Wote wanatikisa vichwa kufuatisha midundo yake. Inavutia sana.

Mpaka unaisha sijakariri neno lolote. Lakini kuna matukio ya video yanajirudia kichwani. Nagundua nimevutiwa na ubora wa video na matukio yake. Natamani kuutazama tena na tena. Naamua kuzama You Tube. Nandy ananikosa kwenye mashairi, ananinasa kwenye video. Na sijutii kutazama.

Baadaye naamua kumsaka na Ruby naye. Kisha natazama video zake kadhaa. Narudia kuzitazama mara kadhaa. Nagundua Ruby ananinasa kwenye sauti na kuimba kuliko video. Pamoja na uwezo wa kuimba ila matukio ya kwenye video zake ni ya kawaida. Ruby ni mnyama kwenye sauti na kuimba.

Nandy anaongoza kwa pointi nyingi. Pamoja na Ruby kutoa nyimbo kadhaa, lakini sioni kivuli chake kando ya Nandy. Tukisimamia ukweli ni kwamba kaachwa maili kadhaa na Nandy. Kuanzia shoo, kusikika kwa nyimbo na kuongelewa mitaani mpaka mitandaoni.

Advertisement

Kwa wawili hawa. ‘Game’ liko kwenye kwapa za Nandy. Likinusa manukato yake. Analiendesha atakavyo. Kuanzia viunga vya Daslama mjini, mikoani hadi nchi jirani. Unaweza kuwa na kipaji kikubwa ukakosa mvuto kwa jamii. Nandy ana kipaji na ana mvuto kijamii. Hii si dhambi. Jay Z na Nas hawa ‘mabraza’ wa Marekani. Wana vipaji, ni wanamuziki wakubwa na wakongwe. Lakini Nas anaeleweka zaidi kwa wana Hip Hop. Wakati Jay Z hata wana kwaya ya Kahama Choir a.k.a “Mkono wake bwana”. Wanaweza wasimuelewe Nas lakini siyo Jay Z.

Juma Nature na ‘vichwa’ vingi vya Bongo Fleva. Vilianza kujulikana miaka ya 2000 lakini Nature akawa maarufu hata nje ya kile walichokifanya. Kwa maana hata muumini wa Kakobe, na mkulima wa mbaazi ilikuwa rahisi kulifahamu jina lake kuliko wenzake.

Alikuwa nyota wa muziki aliye kwenye uhusiano’ na muigizaji nyota. Uwepo wa Sinta kando yake ulimpaisha katikati ya wenzake. Alivunja daraja la mipaka na kufuatiliwa hata na ‘beki tatu’, anayemfuatilia Sinta kwenye kundi la sanaa la Kaole. Nature akawa ana uzito zaidi ya wenzake.

Kabla ya Ufalme wa Rhymes, Afande Sele hakuwa daraja moja na Nature au Prof Jay. Huo ndio ukweli. Ushindi wake wa Mfalme wa Rhymes ukampaisha, kutoka mashabiki wa michano na mashairi yake tu. Mpaka kumiliki utajiri wa mashabiki toka kila upande.

Ufalme wa Rhymes kwa Sele na uhusiano wa Nature kwa Sinta. Ukafanya waongeleke zaidi ya kina Solo Thang, Soggy Doggy na wenzao. Ndivyo ilivyo kwa Jay Z baada ya kumiliki mwili wa Beyonce. Akaanza kuhusudiwa hata na jamii ambayo haina vinasaba na ngoma ngumu za kufoka.

Unapoongelewa sana na umaarufu huongezeka. ‘No mata’ unaongelewa kwa lipi. Hata Hitler ni maarufu ingawa umaarufu wa kifedhuli. Mwanzo tuliaminishwa Nandy dizaini anabebwa na mbeleko ya Ruge. Lakini baada ya mchizi “kuresti ini pisi’ mtoto kafanya makubwa zaidi. Hakuna uchawi zaidi ya ‘kujibrand’ kwa matukio na mbwembwe za hapa na pale. Ndilo bao kubwa la Nandy.

Nas aliamini michano tu. Jay Z akajiongeza kibiashara. Hata kama hili hakupanga, lakini uwepo wa Beyonce kando yake ulisaidia. Nas ungempata kimashairi na michano. Jay Z kimichano, kibiashara na hata shepu ya Beyonce. Akawa na upana wa kuongeleka.

Narudia unapoongelewa zaidi ndivyo unavyopata umaarufu zaidi. Na umaarufu wa lisilo baya kwa jamii huleta pesa mkononi. Kwenye hili Nandy anamficha Ruby. Si kwa video yake na Billnas tu. Si kwa kifo cha Ruge kilichofanya tujue walikuwa wachumba.

Nandy amekuwa rahisi kuongeleka kuliko mwenzake. Imefikia wakati ili ‘atrendi’ labda aongelee lolote kuhusu Nandy. Lakini Nandy hahitaji kumuongelea Ruby ili ‘atrendi’, anajitegemea zaidi, amekuwa rafiki wa ‘peji’ za insta kuliko Ruby. Ni kama Jay Z na Nas.

Ruby kiuwezo ni mkali zaidi ya Nandy. Na Nandy alipita njia za Ruby ili afikie hapo alipo kisanaa. Lakini mchezo wa Nandy hivi sasa ni mtamu kuliko wa Ruby. Wakati Ruby anaamini katika ubora wake kisanaa. Nandy anajiongeza ili afanye biashara zaidi. Na ‘ofu cozi’ kafanikiwa sana. Tofauti iliyopo ni kwamba. Nandy hakuona aibu kupita njia za Ruby ili afike pale alipo kisanii. Ruby haamini katika njia za Nandy kupiga pesa zaidi. Anaumizwa na walioshauri Nandy apite njia zake kuliko kufurahia ushauri wa kutaka afanye analofanya Nandy hivi sasa ili apige pesa.

Ruby nje ya ubora wake kimuziki hana zaidi la kuongelewa. Nandy ana mengi ya kuongeleka kuliko ubora wa muziki wake. Ndo maana anageuka lulu mpaka kwenye uigizaji. Ndo maana anakuwa mtu rafiki wa media. Ruby anatakiwa ajivue joho la umimi kisha ajiachie.

Wapo wengi wasioelewa kwamba kipaji cha muziki ni jambo moja na usimamizi wa kipaji hicho ni jambo lingine. Kuna kipaji cha muziki na uwezo wa kusimamia wanamuziki. Nandy alisimamiwa na kuonyeshwa njia akaikariri. Ruby aliishia kutengeneza ‘jingo’ akasepa.

Wapo wanaodai Ruby ni kiburi. Siamini katika hilo. Kiburi chake hakiwezi kunifanya mimi nishindwe kupiga pesa kupitia yeye. Kwenye muziki kitu hatari zaidi ni kukosa uvumilivu. Ruby hakuwa mvumilivu pengine kwa kuamini katika kipaji zaidi.

Hata uwe na kipaji kikubwa kiasi gani. Kama huna usimamizi imara utaishia hewani kama upepo. Wasanii wengi waliopo mitaani wanakata tamaa ya muziki, wanakosa uvumilivu. Hata kutumia pesa hovyo ni kukosa uvumilivu wa kuacha pesa benki zizaliane.

Hawakutaka kuvumilia kutazama pesa kabatini. Wakataka kaunta za pombe na ‘totozi amazing’ za mjini wazikomeshe. Kabla ya Ruby wapo wengi walipita kwenye mikono ya Ruge. Na kabla ya Nandy wapo waliofanikiwa sana kupitia Ruge. Uvumilivu tu na inategemea uvumilivu kwa lipi.

Sauti ya Ruby kwenye matangazo ilikuwa maarufu kuliko sura. Aliposepa mikononi mwa Ruge na matangazo yakasepa. Hivi sasa Ruge hayupo ambaye pengine alifanya Nandy awe juu yake. Ni wakati wake sasa kuionyesha dunia kama kipaji ni zaidi ya usimamizi wa Ruge.

Nandy sina shaka kwake. Maana kwa muda mfupi kaonyesha anaweza nje ya mikono ya Ruge. Lakini ataweza kuendelea kusimama bila uwepo wa sapoti ya Ruge? Kinamchomsaidia ni kuwa mbali ya kipaji, kaonyesha nidhamu ya kusimamiwa.

Hii ndo tofauti yake na Ruby. Kwake anaweza kujitokeza haraka mtu kumsimamia. Wakati Ruby ana jukumu la kuthibitisha kama tuhuma za kiburi ni uzushi au kweli. Ngumu kuwekeza kwa mtu wa aina yake. Asiwe mfano hai wa “Kipaji na maisha ya ovyo ni pacha.” Achana na Nandy na Ruby, kuna Fiesta. Mwaka jana Ruge akipigana uhai wake Afrika Kusini. Tamasha la Fiesta liliyumba kama nyumba iliyopitiwa na ‘greda’. Kuna kazi kuthibitisha kuwa bila uwepo wa Ruge tamasha hilo linafanyika kwa ubora uleule.


Advertisement