Obama awaombea msaada waliokumbwa na mafuriko Msumbiji

Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama

Muktasari:

  • Umoja wa Mataifa umesema wengi wa raia katika mji wa Beira wamejihifadhi kwenye mapaa ya nyumba.

Washington, Marekani. Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama amewataka Wamarekani na wananchi wa dunia kusaidia familia zilizoathirika na mafuriko katika eneo la Magharibi ya kati ya nchi hiyo na wale waliopigwa na Kimbunga Idai Kusini mwa Afrika.

Katika ujumbe wake wa tweet mbili zilizounganishwa kwenye akaunti yake rasmi Obama alijumuisha makala zinazoonyesha njia tofauti ambazo zinaweza kuwasaidia waathirika wa majanga hayo.

'' Adha na mateso yanayojitokeza katika pande mbili za dunia kunahitaji ushirikiano na nguvu kutoka kwetu sote,'' umesomeka sehemu ya ujumbe wake huo wa tweet na kuendelea: “Na hapa kuna njia zingine za kuwasaidia waathirika wa dhoruba nchini Msumbiji, Malawi na Zimbabwe,”.

Wakati huohuo, vikosi vya uokoaji nchini Msumbiji vinahofia kwamba maelfu ya watu wanaweza kuwa wameathirika na mafuriko makubwa yaliyosababishwa na Kimbunga Idai.

Mratibu wa huduma za dharura wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Pedro Matos amesema huenda kuna idadi kubwa ya watu waliokimbia ama waliokwama eneo Beira ambako maelfu ya raia walikuwa wakiishi na kuongeza kuwa waokozi hivi sasa wanajikita zaidi katika operesheni za uokoaji.

Akiwa mjini Geneva, Uswisi msemaji wa WFP, Herve Verhoosel amesema zaidi ya watu 100,000 katika eneo la Manica wanashindwa kupelekewa misaada kutokana na kuharibika kwa barabara zinazoliunganisha eneo hilo na mengine.