PBZ yamwaga misaada ya vifaa vya afya ikiwemo mashine za uchunguzi

Wednesday August 14 2019

Watendaji wa Wizara ya Afya pamoja na wa Benk

Watendaji wa Wizara ya Afya pamoja na wa Benk ya Watu wa Zanzibar wakionesha moja ya shuka zilizokabidhiwa kwa uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar, ikiwa ni msaada kutoka Benk ya Watu wa Zanzibar, Picha na Haji Mtumwa. 

By Haji Mtumwa, Mwananchi [email protected]

Unguja. Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) leo Jumatano Agosti 14, 2019 imekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali ikiwa mashine za uchunguzi wa chembe chembe za damu, vitanda, mashuka na magodoro kwa uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar.

Akikabidhi vifaa hivyo katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Mjini Unguja, Mkurugenzi wa PBZ, Khadija Shamye amesema vifaa hivyo vimegharimu zaidi ya Sh85.5 milioni.

Amesema PBZ imelazimika kutoa msaada huo kwa wizara ya afya kupitia hospitali zake, kutokana na sekta hiyo ni moja ya sekta muhimu inayotumiwa na wananchi wengi walio wanyonge ambao tegemeo lao ni hospitali za Serikali.

Amesema kwa upande wao watazidi kuunga mkono jitihada za wizara ya afya katika kuhakikisha suala la utoaji wa tiba bora kwa wananchi linaweza kufanikiwa siku hadi siku, kama lilivyo lengo la Serikali Kuu chini ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Halima Maulidi Salum ameupongeza uongozi wa PBZ kwa juhudi zao hizo za kusaidia sekta ya afya ambayo ni sekta muhimu katika maisha ya mwanadamu.

Amesema kati ya mashine mbili za uchunguzi wa chembe chembe wa damu walizokabidhiwa moja itapelekwa Hospitali ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja na nyengine itapelekwa Hospitali ya Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo vifaa vingine ikiwa magodoro 50, vitanda 50 pamoja na mashuka 50, vitagaiwa katika hospitali za wilaya zote za Unguja.

Advertisement

Amesema kuja kwa vifaa hivyo anaamini wazi kuwa itakuwa ni moja ya mambo yatakayoongeza nguvu kwa madaktari katika utoaji wa huduma kwa wateja hasa kupitia hizo mashine ambazo kwa kipindi kirefu Hospitali hizo zilikuwa na ukosefu wa  mashine hizo.

“Kilichobaki sasa ni kwa madaktari husika watakabidhiwa jukumu la usimamizi wa vifaa hivyo kuwa waangalifu pamoja na kuzitunza ili kuweza kutumika kwa muda mrefu katika utoaji wa huduma kwa wananchi wetu,” amesema.

Advertisement