Polepole akemea makundi CCM Arusha

Muktasari:

Wanachama wa CCM mkoani Arusha wametakiwa kuachana na migogoro na makundi ili kuwa mfano kwa mikoa mingine nchini.


Arusha. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Humphrey Polepole ameutaka uongozi wa chama hicho mkoa na wilaya kuacha makundi yasiyo na tija kwa chama na taifa kwa ujumla.

Akizungumza katika mkutano wa halmashauri kuu ya wilaya ya Arusha jana, Polepole alisema amepata taarifa za kuwepo migogoro ambayo inafaa kuondolewa ili kufanikisha mshikamano wa chama hicho.

"CCM imepata mafanikio katika kipindi cha miaka 42 iliyopita lakini hatuwezi kuwazuia wanaobeza mafanikio yetu kwa sababu kubeza ni kipaji walichojaliwa, sisi tusonge mbele na tuondoe tofauti zetu," alisema.

Alisema uzoefu wake unaonyesha migogoro huwa haisababishwi na wanachama ambao ndio watafutaji wa kura bali huchochewa na viongozi wenye maslahi yao binafsi.

"Hivi nyie wanachama wenzangu hamjui CCM ikiharibikiwa tunachelewesha maendeleo ya taifa letu kwa sababu za viongozi wachache wenye maslahi yao binafsi," alisema Polepole.

Bila kumtaja majina, Polepole alisema mwaka 2020 ajiandae kufanya kazi nyingine kwa sababu hatapata ridhaa ya wananchi kuchaguliwa tena bali atafute kazi nyingine.

"Nimetembelea miradi ya maendeleo kwenye kata mbalimbali hayupo kabisa amehamishia jimbo kwenye mikoa mingine na kwenye mitandao mpeni salamu zangu," alisema Polepole. 

Naye mwenyekiti wa CCM kata ya Elerai, Peter Kasela "Majeshi" alisema kumekua na mkanganyiko wa viongozi wa chama kuingiliana majukumu na viongozi wa Serikali jambo linalokwamisha utendaji kazi.