Polisi: Hatujamkamata Mdude Chadema

Sunday May 5 2019

Mwanachama wa Chadema, Mdude Nyagali maarufu

Mwanachama wa Chadema, Mdude Nyagali maarufu Mdude Chadema 

By Godfrey Kahango, Mwananchi [email protected]

Mbeya. Wakati taarifa zikisambaa mtandaoni  kuwa mwanachama wa Chadema, Mdude Nyagali maarufu Mdude Chadema ametekwa na watu wasiojulikana akiwa ofisini kwake Vwawa-Mbozi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando amesema hana taarifa kuhusu tukio hilo.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi leo Jumapili Mei 5, Kamanda Kyando amesema taarifa ya kukamatwa kijana huyo hajazipata na kwamba hakuna milio ya risasi iliyosikika katika maeneo hayo.

"Mimi ni mkazi wa eneo linalodaiwa kuwa risasi zimepigwa lakini sijasikia na kama unavyojua mji wa Vwawa ni mdogo ambao zikipigwa risasi lazima utasikia," amesema.

Hata hivyo, Kamanda Kyando amesema ataendelea kufuatilia kwa kina zaidi juu ya taarifa hizo na kwamba baadaye leo huenda ukweli ukajulikana.

Akizungumza na Mwananchi, Mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga amesema: “Kweli Mdude ametekwa na watu waliokuwa kwenye magari mawili, Nissan Patrol na Landcruiser na walifika ofisini kwake mjini Vwawa-Mbozi. Na hadi sasa  sijui yuko wapi.”

Amesema tukio hilo limetokea jana saa 12 jioni na baada ya tukio hilo amewasiliana na Kamanda Kyando lakini amejibiwa kwamba hana taarifa hizo na wao (polisi) hawajamkamata.

Advertisement

“Nimezungumza na RPC ameniambia hawajui na siyo wao waliomkamata. Lakini pia nimetoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Nicodemas Mwengela kuhusiana na tukio la kutekwa kwa Mdude,” amesema Haonga.

Haonga amesema mbali na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola lakini pia ametoa taarifa kwa uongozi wa juu wa Chadema na wanaendelea kufuatilia kwa karibu juu ya tukio hilo ili kujua Mdude amechukuliwa na watu gani na amepelekwa wapi.

 

Advertisement