UTAWALA BORA; Polisi lawamani kamatakamata ya wapinzani

Dar es Salaam. Wakati kasi ya kukamata wanasiasa wa upinzani ikiongezeka, Jeshi la Polisi limesema halistahili lawama kwa kuwa linatekeleza wajibu wake.

Wabunge wawili wa Chadema, Suzan Kiwanga (Mlimba) na Peter Lijualikali waliingia tena katika orodha ndefu ya wabunge wa chama hicho waliokumbana na kadhia hiyo baada ya kukamatwa juzi kwa makosa ambayo awali yalikosa ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani.

Wabunge hao ambao walinyimwa dhamana, wamekamatwa katika kipindi ambacho wabunge wenzao, Halima Mdee (Kawe) na Joseph Mbilinyi pia wamekumbwa na kamatakamata hiyo katika maeneo tofauti, wote wakidaiwa kutoa maneno ya uchochezi.

Na kwa kuangalia miaka mitatu nyuma, kuna orodha ndefu ya wabunge wa chama hicho waliokamatwa na wengine kufunguliwa mashtaka, akiwemo mwenyekiti Freeman Mbowe, ambaye yuko mahabusu baada ya kufutiwa dhamana.

Lakini, pamoja na orodha hiyo kujumuisha zaidi ya wabunge 20 wote kutoka upinzani, msemaji wa Jeshi la Polisi, Ahmed Msangi alisema wanaokamatwa ni wale wanaotenda makosa.

“Polisi wanakamata mtuhumiwa aliyefanya kosa kutokana na makosa yake. Hatukamati mtu yeyote tu, hatuonei mtu,” alisema Msangi.

Mbowe na mbunge wa Tarime, Esther Matiko walifutiwa dhamana katika kesi waliyoshtakiwa pamoja na viongozi wengine wa Chadema wakituhumiwa kufanya makosa 13 ya uchochezi, uasi na kuhamasisha wafuasi wao kutenda makosa.

Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ya jinai namba 112/2018 ni Dk Vincenti Mashinji ambaye ni katibu mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu na John Mnyika (manaibu katibu wakuu Zanzibar na Bara), Mdee (Kawe), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na John Heche (Tarime Vijijini).

Mbali na kesi hiyo baadhi ya viongozi na wengine wanakabiliwa na kesi nyingine tofauti katika mahakama mbalimbali nchini.

Kesi hizo zimemshangaza Profesa Abdallah Safari, makamu mwenyekiti wa Chadema.

“Mbona viongozi wa CCM hawakamatwi? (Kwanini) ni wapinzani tu? Uliona lile tamko la EU? Ndiyo hayo yaliyoelezwa. Waulizeni CCM,” alisema alipohojiwa na Mwananchi kuhusu hali hiyo.

Alikuwa akirejea tamko la Umoja wa Ulaya (EU) la mwaka jana lililolaani uendeshaji wa siasa nchini likisema kuna ukandamizwaji wa haki za binadamu na uminywaji wa demokrasia.

EU ilisema hali hiyo inaifanya iamue kupitia upya sera yake ya uhusiano na Tanzania, ikiwa ni katika kipindi ambacho aliyekuwa balozi wake nchini, Roeland De Geer aliondoka nchini.

Kutokana na matukio hayo, wakili Awadhi Said wa Zanzibar alisema hali hiyo inatokea kwa sababu nchi imekosa taasisi imara za kusimamia sheria na haki.

“Kufanya siasa ni moja ya haki za binadamu na haki hizo zimewekwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” alisema.

“Tatizo hatujawa na taasisi imara za kusimamia haki hizo. Tunategemea uamuzi wa mtu mmoja, akipenda demokrasia nchi inakuwa hivyo, asipopenda demokrasia inaminywa.”

Huku akisisitiza kutekelezwa kwa haki za siasa, Awadhi amevishauri vyombo vya dola kulinda imani ya wananchi kwani wakivichoka amani inaweza kutoweka.

“Unazuia vyama vya siasa vizifanye siasa hadi wakati wa uchaguzi. Kazi ya chama cha siasa ni kueneza sera si kufanya chaguzi tu,” alisema.

“Maandamano ni haki ya wananchi. Ukifanya vizuri wataandamana kukupongeza, ukifanya vibaya wataandamana kupinga.

“Taasisi hizi za haki zinapaswa kulinda imani ya wananchi. Wewe unasema hukamati wapinzani, lakini wananchi wanaona... Nchi zilizoingia kwenye machafuko ni kwa sababu wananchi walichoshwa na taasisi za kulinda haki na sheria.”

Hata hivyo, naibu katibu mkuu wa CCM (Bara), Rodrick Mpogolo alisema hakuna upendeleo unaofanywa na vyombo vya dola kwa chama hicho tawala. “Kukamatwa kunategemeana na kuvunja sheria. Sasa mtu atakamatwa kama hakufanya kosa?” alisema.

“Sidhani kama kuna upendeleo. Kuhusu kukamatwa ni suala la makosa, unafanya makosa ndiyo unakamatwa.”

Novemba 27, 2018 wakati wa ufunguzi wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais John Magufuli aliwaonya wapinzani kuwa wasipoheshimu sheria wataishia magerezani.

Matukio ya kamatakamata

Katika matukio ya hivi karibuni, Mdee, ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) alilazwa mahabusu baada ya kujipeleka kuhojiwa na kituo cha polisi cha Oysterbay alikoitwa baada ya kutuhumiwa kutoa maneno ya uchochezi.

Kushikiliwa kwa Mdee kulikuja siku chache baada ya mbunge wa Mbeya Mjini kuhojiwa kwa saa kadhaa, akituhumiwa kutoa maneno ya uchochezi alipokuwa akijadiliana na wananchi kuhusu utaratibu wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo.

Mkoani Morogoro, Kiwanga na Lijualikali wamefufuliwa kesi yao ya mwaka juzi na kusomewa mashtaka manane yanayohusu vurugu na kuchoma moto ofisi ya serikali ya mtaa wakati wa uchaguzi mdogo.

Mbunge wa Arusha Mjini Lema naye aliwahi kusota rumande ya gereza la Kisongo kwa miezi minne kwa kosa la uchochezi.

Lijualikali, ambaye amekumbana na misukosuko kadhaa ya polisi tangu ashinde ubunge kwa mara ya kwanza mwaka 2015, na Kiwanga, walishikiliwa na polisi kwa takriban siku sita kabla ya kufikishwa mahakama juzi.

Lijualikali pia aliwahi kuhukumiwa kifungo, lakini akatolewa kwa rufaa.

Mwingine aliyewahi kutumikia kifungo ni Joseph Mbilinyi au Sugu, mbunge wa Mbeya Mjini ambaye alipatikana na hati ya kutoa maneno yasiyofaa dhidi ya Rais.

Wengine wenye kesi ni pamoja na Tundu Lissu (mbunge wa Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Zitto Kabwe, ambaye ni kiongozi wa ACT Wazalendo.

Wengine waliopata misukosuko ni aliyekuwa waziri mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Edward Lowassa, ambaye aliitwa kuhojiwa na kutakiwa kuripoti polisi kutokana na kauli zake kuhusu viongozi wa kundi la Uamsho.