Profesa Kabudi azungumzia haki ya tendo la ndoa kwa wafungwa

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi akijibu hoja za wabunge waliochangia katika Taarifa ya Kamati mbili za Kudumu za Bunge, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo bungeni jijini Dodoma jana. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema suala la kuwakutanisha wafungwa na wenza wao kwa Tanzania halina ulazima na baada ya utafiti walibaini haliwezekani

Dodoma. Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema suala la kuwakutanisha wafungwa na wenza wao kwa Tanzania halina ulazima kwa kuwa halivunji haki za msingi.

Profesa Kabudi alitoa kauli hiyo leo jioni Ijumaa Februari 8, 2019 wakati akichangia taarifa za kamati za Bunge za Sheria na Sheria Ndogo kwa mwaka 2018.

Amesema Tanzania ilifanya utafiti na walibaini kuwa jambo hilo haliwezekani.

"Hata mataifa ya wenzetu huko si kwamba wenza wanakwenda magerezani hapana, bali wana utaratibu mwisho wa mwaka wafungwa wanaotembelea familia zao majumbani na kukaa hadi Januari 2 ndio wanarudi gerezani, " alisema Kabudi.

Amesema wenza wakienda magerezani hata faragha haitakuwepo kwani kila mmoja atajua wanachofanya hivyo usiri hautakuwepo huku akisisitiza uvumilivu kwani kuna wanaume rijali lakini wamekubali kuwa waseja.

Leo bungeni kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria imeishauri Serikali kuandaa na kutekeleza mpango mkakati chini ya Magereza kuwafanya wafungwa wanapata haki ya kutembelewa na wenza wao na kupata haki ya tendo la ndoa.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kamati hiyo mwenyekiti wake, Mohamed Mchengerwa amesema hatua hiyo itapunguza maambukizi ya magonjwa kwenye magereza ikiwemo Ukimwi.

“Serikali iandae na kutekeleza mpango mkakati chini ya Magereza utakaohakikisha wafungwa wenye ndoa wanawekewa mazingira yatakayohakikisha wanapata haki ya kutembelewa na wenza wao na kupata haki ya tendo la ndoa kwa kuzingatia utaratibu utakaowekwa na mamlaka husika,” amesema.