VIDEO: Profesa Lipumba ashinda nafasi ya uenyekiti CUF

Muktasari:

Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Thenei Ally Juma amesema kuwa Profesa Lipumba ameshinda kwa kupata kura 516.

Dar es Salaam. Profesa Ibrahim Lipumba ameshinda nafasi ya uenyekiti wa CUF Taifa.

Lipumba ameshinda leo Machi 13, 2019 kwenye uchaguzi mkuu wa saba wa chama hicho uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Akitangaza majina ya washindi katika uchaguzi huo, mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Thenei Ally Juma amesema Lipumba amepata kura 516 sawa na asilimia 88.9.

Hata hivyo, haikuelezwa ni kura ngapi zimepigwa. Lakini ukumbi ulikuwa na jumla ya wajumbe 598.

Amemtaja aliyeshinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara kuwa ni Maftaha Nachuma aliyepata kura 231 sawa na asilimia 40.9.

Juma amemtangaza pia Abbas Juma Muhunzi kuwa mshindi wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar baada ya kupata kura 349 sawa na asilimia 60.9.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Profesa Lipumba amesema walioshinda ni vijana wake na hana tabu nao.

“Nitafanya nao kazi, wengi wao wameulizwa kushika nafasi hizo jana na leo wameshiriki na wameshinda,” amesema Lipumba.