RIPOTI YA CAG: Macho, masikio bungeni Dodoma

Monday April 8 2019

 

By Daniel Mjema na Taus Ally, Mwananchi [email protected]

Moshi/Dar. Kama ni kugonga vichwa vya Watanzania maeneo mbalimbali katika kipindi cha wiki moja basi ni suala la Bunge kuazimia kutofanya kazi na Profesa Mussa Assad, ambaye ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Licha ya uamuzi huo kufikiwa Jumanne iliyopita, sasa macho na masikio yanaelekezwa kwa chombo hicho cha kutunga sheria ikiwa ni saa 72 zimebaki kabla ya siku ya mwisho ya ripoti hiyo kukabidhiwa na kupokewa.

Azimio hilo lilitokana na CAG huyo kutuhumiwa kulidhalilisha Bunge kwa kuliita ‘dhaifu’ hivyo Spika Job Ndugai kuiagiza Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumhoji na taarifa ya kamati ilipowasilishwa bungeni ilimkuta na hatia.

Kauli hiyo aliitoa wakati alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa (UN) akiwa New York, Marekani alikokuwa akihudhuria mkutano.

Alitumia neno ‘udhaifu’ wa Bunge alipokuwa akieleza sababu za kutofanyiwa kazi ripoti zake ambazo zimekuwa zikibainisha ufisadi katika maeneo kadhaa.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari Alhamisi iliyopita, Spika Ndugai akijibu swali aliloulizwa ikiwa ripoti hiyo ikipelekwa ataipokea au la hasa ikiwa na saini ya Profesa Assad, alisema, “Kitu ambacho sijaletewa kwa nini nianze kufanya mpango na wewe.”

Advertisement

“Kusema kwamba kikija hivi itakuwa hivi, hicho kitu mimi sina mkononi, kwa nini tuongelee hypothesis niseme ndio au sio. Kasome Katiba inasemaje, Katiba imesema kila kitu kuhusu hilo eneo,” alisema Ndugai.

“Habari ya saini hilo halinihusu, sisi hatufanyi kazi na Profesa Assad kama una mengine utajijibu mwenyewe sasa. Anayetudharau sisi (Profesa Assad), kule Kongwa (jimbo analoliongoza) wananiamini mtu kaaminiwa na watu mheshimu na mpe haki yake,” aliongeza Ndugai.

Tayari Profesa Assad amekwisha iwasilisha ripoti yake kwa Rais John Magufuli, na kiutaratibu hutakiwa kuwasilishwa bungeni ndani ya siku saba tangu Bunge lilipoanza.

Mkutano huo wa 15 wa Bunge la Bajeti ulianza Aprili 2 na siku saba hizo zinamalizika keshokutwa Aprili 10, ambazo ni saa 72 kuanzia leo Jumatatu.

Maoni ya Dk Bana

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana amesema bado kuna nafasi ya Profesa Assad kufuta kauli yake ili kumaliza mvutano huo.

Dk Bana aliliambia Mwananchi jana kuwa alipokosea CAG ni kutofuta kauli yake kuonyesha utii katika utumishi wa umma ambao unasisitizwa mara zote.

“Hili jambo lilitakiwa kumalizwa mapema sana. Alipoitwa na kamati ya Bunge, CAG alitakiwa kutengua kauli yake. Angeomba kufuta kauli yake bila shaka angeeleweka na ingemsaidia kuepuka kulumbana na wanasiasa ilhali yeye ni msomi mzuri,” alisema Dk Bana.

Kwa kuliita Bunge dhaifu, alisema haikubaliki na hata angefanya hivyo kwa Freeman Mbowe kwa mfano, amuite dhaifu kwa maelezo ameshindwa kuiongoza Chadema angeshambuliwa sana.

Alisema kwa kuwa uteuzi wa CAG Assad unakamilika Novemba basi avumiliwe mpaka kipindi hicho kwani inaeleweka Bunge haliwezi kurudi naye tena mezani.

“Alichokisema kilikuwa kimeshaufikia umma kilichotakiwa ni kulegeza msimamo. Bado anayo nafasi ya kufanya hivyo badala ya kuwa na msimamo mkali,” alishauri Dk Bana.

Kura mtandaoni

Taasisi ya Change Tanzania ambayo mara baada ya azimio hilo kupitishwa, walianzisha ukusanyaji wa kura kulipinga.

Kura hizo za mtandaoni zilizoanza Aprili 3 kupitia mtandao wao, walikuwa na lengo la kukusanya kura 17,500 za kuazimia kulitaka Bunge lifute azimio lake.

Hadi jana saa 2.50 usiku, jumla ya kura 15,320 zilikuwa zimepigwa katika mtandao huo.

Maandamano ya amani

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Karama Kaila alisema wanalitaka Bunge kuweka kwenye shughuli za Bunge (Order Paper) upokeaji wa taarifa ya CAG ikiwa na saini ya Profesa Assad ifikapo keshokutwa Aprili 10.

Alisema wametoa taarifa kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Dodoma kuhusu kufanyika kwa maandamano hayo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alipoulizwa na Mwananchi jana alisema hajawapa taarifa za kufanyika kwa maandamano hayo.

Maoni ya wanasheria

Wakili wa Kujitegemea, Frank Robert alisema nafasi ya CAG ni ya kikatiba na ofisi ya CAG ni watu huru na hawawajibiki kupokea maagizo kutoka serikalini.

“CAG na ofisi yake ni watu huru, hawawajibiki kupokea ushauri au maelekezo ya ofisi yoyote ya Serikali isipokuwa kama kutakuwa na jambo la kimahakama kwa mujibu wa ibara ya 143(6)”alisema.

“CAG pamoja na kufanya kazi kwa niaba ya Bunge, lakini hawajibiki moja kwa moja kwa Bunge. Sheria inamtaka akishafanya kazi yake akabidhi ripoti yake kwa Rais na ameshafanya,” alisisitiza.

Wakili mwingine, Peter Mshikilwa alisema sheria inasema CAG atakabidhi ripoti zake za mwaka kwa Rais ambaye atawasilisha kwenye Bunge na kuwa nyaraka ya umma.

“Msingi wake kikatiba Rais ni sehemu ya Bunge, lakini CAG hawajibiki kwa Bunge. Bunge kukataa kufanya kazi na CAG maana yake ni kukwepa kutekeleza jukumu lake la kuisimamia Serikali,” alisema.

Rais wa zamani wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Fatma Karume alisema CAG hawezi kuondolewa na Rais wala Bunge, bali Rais anachopaswa ni kuunda jopo la majaji kumchunguza.

Juzi, Profesa Assad alilieleza gazeti la The Citizen kuwa hajui sababu zilizosababisha Bunge lifikie uamuzi wa kutoshirikiana naye

“Kumekuwa na tuhuma kwamba niliita Bunge kuwa ni dhaifu, lakini hizo hazina msingi. Nilifanya mahojiano hayo wakati nilipotembelea Umoja wa Mataifa, ambao Tanzania ni mwanachama.” alisema ambaye aliteuliwa kushika nafasi hiyo mwaka 2014.

“Nikiwa Umoja wa Mataifa, nilihojiwa na idhaa ya Kiswahili na mwandishi wa habari Mtanzania ambaye aliibua masuala yanayoihusu Tanzania. Kwa hiyo haitakuwa sahihi kusema nilikuwa nazungumzia mambo ya ndani nikiwa katika ardhi ya nje.”

Advertisement