RPC aliyetenguliwa na Waziri Lugola akamata noti bandia

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,Ramadhani Ng’anzi akionesha waandishi wa habari jana noti za fedha bandia zilizokamatwa kwenye operesheni za kutokomeza uhalifu jijini Arusha. Picha na Filbert Rweyemamu

Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Ramadhan Ng’anzi, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ameonekana kuendelea na wadhifa wake na jana alizungumzia kukamatwa kwa watuhumiwa wanaojihusisha na utengenezaji wa noti bandia.

Januari 16, Lugola alitengua uteuzi wa makamanda wa polisi wa mikoa mitatu; Salum Hamduni (Ilala), Emmannuel Lukula (Temeke) na Ramadhan Ng’anzi (Arusha).

Lakini, jana Kamanda Ng’anzi alionekana akiendelea na kazi yake kama kawaida na alizungumzia ukamataji wa noti bandia mkoani Arusha.

Huku makamanda hao watatu wakiendelea na kazi licha ya uteuzi wao kutenguliwa, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amesema atafanya mabadiliko wakati wowote wa makamanda wa polisi wa mikoa ya Ilala, Temeke na Arusha.

Kwa mujibu wa Lugola, sababu za kutengua uteuzi wa makamanda wa Ilala na Temeke ni kushindwa kusimamia mianya ya rushwa na utoaji wa dhamana kwa watuhumiwa, huku Ng’anzi akidaiwa kumwadhibu askari aliyetoa orodha ya polisi wanaojihusisha na biashara haramu ya bangi na mirugi wakati wa ziara ya naibu waziri wa wizara hiyo, Hamad Masauni.

IGP Sirro jana alizungumza na Mwananchi kuhusu utekelezaji wa agizo hilo la Lugola. “Bado nalifanyia kazi agizo lake na wakati wowote nitafanya mabadiliko ya makamanda wa mikoa hiyo kama ilivyoagizwa.”

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, Ng’anzi alisema polisi iliwakamata watuhumiwa sita kwa makosa mbalimbali, kati yao wanne ambao hakuwataja majina wanajihusisha na utengenezaji wa fedha bandia.

Alisema mtuhumiwa wa kwanza alikutwa na idadi ya noti bandia za Dola za Marekani 50 ambazo zingekuwa halali zingekuwa na thamani ya dola 500.

Alisema mtuhumiwa huyo alipohojiwa aliwapeleka polisi nyumbani kwake zilipokutwa fedha hizo na watuhumiwa wenzake wakakamatwa.

“Huyu mtuhumiwa wa kwanza aliwapeleka askari wetu nyumbani kwake eneo la Daraja Mbili ambako zilikutwa fedha bandia za mataifa mbalimbali, tunaendelea kuwahoji ili tung’oe mtandao mzima wa uhalifu huu,” alisema Ng’anzi

Alitaja noti hizo bandia kuwa ni dola za Marekani, fedha za Umoja wa Ulaya (Euro), Kenya, Malawi, Zambia, Rwanda, Afrika Kusini, Angola na Sudan.

Kati ya fedha hizo bandia zipo Dola za Marekani 120,000 na Euro 10,700.

Alisema watuhumiwa hao wanashikiliwa kwa mahojiano na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani.

Ng’anzi alisema watuhumiwa wengine wawili, Kennedy Mbilinyi na Richard Loishiye wamekamatwa kwa kuiba gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 241 DKC na kujaribu kulivusha mpaka wa Namanga kuingia Kenya.

Alisema mmiliki wa gari hilo alikuwa akitafuta mnunuzi na siku ya tukio alikuwa ameliegesha kwenye maduka ya TFA wakati akifanya manunuzi na alipotoka nje hakulikuta.

Katika tukio jingine, Kamanda Ng’anzi alisema katika operesheni iliyofanywa na polisi jijini hapa wamefanikiwa kukamata pikipiki nne zilizokuwa zikitumiwa na vijana wanaojiita “Tatu Mzuka” wanaojihusisha na upokonyaji wa pochi za wanawake.

“Tumekamata pia vifaa mbalimbali ambavyo ni kompyuta, televisheni na vifaa vingine vya nyumbani,”alisema Ng’anzi ambaye hakuwa tayari kuzungumzia kutenguliwa kwake kulikofanywa na Waziri Lugola.

Kuhusu makamanda wa mikoa mingine waliotenguliwa kuwepo kazini, Mwananchi lilimtafuta kamanda wa Ilala na simu yake ya mkononi ilipokelewa na msaidizi wake aliyeeleza kuwa kamanda huyo yupo kwenye kikao.

Kamanda wa Temeke, Emmanueli Lukula alipogiwa simu na mwandishi wa gazeti hili ilipokelewa na msaidizi wake na kumfahamisha kuwa yuko kikaoni

“Ameingia muda si mrefu, labda umpigie baada ya masaa mawili watakuwa wamemaliza ataweza kukusikiliza shida yako,” alisema msaidizi huyo.