Radi yajeruhi wanafunzi 14 Kagera

Dr George Kasibante akihudumia mmoja wa wanafunzi waliojeruhiwa na radi

Muktasari:

  • Wanafunzi 14 wa shule ya sekondari Rulongo wilayani Muleba Mkoa wa Kagera wamelazwa katika hospitali ya Lubya wilayani humo baada ya kujeruhiwa na radi

Muleba. Wanafunzi 14 wa shule ya sekondari Rulongo wilayani Muleba Mkoa wa Kagera wamelazwa katika hospitali ya Lubya wilayani humo baada ya kujeruhiwa na radi.

Akizungumza leo Jumatano Januari 16, 2019 mganga mkuu wa hospitali hiyo, George Kasibante amesema tukio hilo limetokea leo na kwamba kati ya wanafunzi hao,  watatu wana hali mbaya baada ya kuungua sehemu kubwa mwilini.

Amesema mwanafunzi mmoja amepoteza fahamu na madaktari wanajitahidi kuhakikisha anarejea katika hali yake ya kawaida, kwamba wengine walipata zaidi mshtuko.

Amesema radi hiyo ilipiga vyumba vya madarasa ya kidato cha pili na tatu, kwamba shule hiyo ipo mlimani eneo ambalo radi hupiga zaidi na kuwashauri wanafunzi kutojikinga na mvua katika maeneo yenye miti mirefu.

"Kawaida radi hupita sehemu yenye miti mirefu na majengo ya namna hiyo lakini tunaomba wazazi na walezi kuamini madaktari kwa huduma zinazoendelea muhimu wanafunzi hawa wawaletee kadi za bima ya afya,” amesema.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Muleba,  Emanuel Sherembi amethibitisha wanafunzi hao kupigwa na radi na kwamba amemuagiza mganga wa wilaya kufuatilia matibabu ya wanafunzi hao.