Rais wa Afrika Kusini atua Tanzania

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa akipokewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius  Nyerere jijini Dar es Salaam jana usiku. Rais Ramaphosa amewasili kwa ziara rasmi ya siku mbili nchini kabla ya kuhudhuria Mkutano wa 39 wa Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC

Muktasari:

  • Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amewasili Tanzania kwa ziara ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, John Magufuli ambapo pamoja na mambo mengine watajadili mambo ya nchi hizo mbili kuelekea Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Dar es Salaam. Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ameingia nchini Tanzania usiku wa kuamkia leo Alhamisi Agosti 15,2019 kwa ziara ya siku mbili kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, John Magufuli.

Ziara hiyo itawawezesha viongozi hao kujadili mambo yanayohusu nchi hizo, Bara la Afrika na mambo ya kimataifa na kujihakikishia wajibu wao katika ushirikiano wa karibu.

Ziara hiyo inakuja zikiwa zimebaki mbili kuelekea mkutano wa kawaida wa 39 wa viongozi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika jijini Dar es Salaam Agosti 17 na 18, 2019 katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere.

Leo Alhamisi Agosti 15, 2019 saa 2: 00 atafanya mazungumzo Ikulu ya Dar es Salaam na mwenyeji wake Rais Magufuli na saa 5 hadi 8 mchana atakuwa ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) kwenye Jukwaa la Biashara.

Ijumaa ya Agosti 16, 2019 saa 3 asubuhi, Rais Ramaphosa atatembelea kambi ya wapigania uhuru Mazimbu mkoani Morogoro.

Mwaka 2011 makubaliano ya kuanzisha tume ya mataifa mawili (BNC) kati ya Tanzania na Afrika Kusini ulisainiwa.

Uzinduzi wa BNC ulifanyika Tanzania mwaka 2017 na nchi ya Afrika Kusini itahodhi mkutano kama huo katika tarehe itakayopangwa.

Tanzania inaagiza bidhaa mbalimbali kutoka Afrika Kusini katika eneo la uzalishaji wa viwanda, mashine, vifaa vya kimakanika, karatasi, bidhaa za mpira, magari, vyuma, teknolojia na huduma.

Kwa upande mwingine, Tanzania inasafirisha Afrika Kusini bidhaa ambazo ni dhahabu, kahawa, korosho na pamba.

Kuna zaidi ya kampuni 170 za Afrika Kusini zinazofanya kazi Tanzania katika nyanja zote za kiuchumi.

Rais Ramaphosa ataambatana na mawaziri akiwemo waziri wa ulinzi, maveterani wa jeshi, waziri wa viwanda na biashara, madini na nishati na usalama wa ndani.

Baada ya ziara hiyo Rais Ramaphosa atauongoza ujumbe wake katika mkutano wa 39 wa viongozi wa SADC.