Rummenigge aionya Bayern kubweteka kama 1981

Mshambuliaji wa kimataifa wa Guinea, Naby Keita akijaribu kupiga tik-tak wakati wa mechi ya kwanza ya hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulkaya baina ya Liverpool na Bayern Munich iliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Anfield.

Muktasari:

Bayern ililazimisha sare ya bila kufungana kama ya jana katika mechi ya kwanza ya michuano ya Klabu Bingwa ya Ulaya mwaka 1981, lakini katika mechi ya marudiano mjini Munich ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na hivyo kutolewa kwa sheria ya bao a ugenini

Karl-Heinz Rummenigge ameionya Bayern Munich kutoruhusu historia kujirudia dhidi ya Liverpool katika mechi yao ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya baada ya timu hizo kwenda sare ya bila kufungana jana usiku.

Bayern ilipata sare hiyo katika mechi iliyofanyika Merseyside na kuwafanya vigogo hao wa Ujerumani kuwa katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kuingia robo fainali wakati timu hizo zitakaporudiana machi 13 kwenye Uwanja wa Allianz Arena.

"Tumefungua mlango kidogo kwa ajili ya mechi ya marudiano, lakini naonya dhidi ya hali ya kubweteka wakati wa kuelekea mechi ya marudiano - si matokeo salama," Rummenigge, mwenyekiti wa Bayern, ameonya.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 63 alikuwa anazungumza kutokana na uzoefu wake wa mazingira kama hayo yaliyowahi kuikuta timu hiyo. Alikuwa kwenye kikosi cha Bayern kama rais wa sasa Uli Hoeness ambacho kilifungwa na Liverpool katika nusu fainali ya michuano hiyo ya Ulaya mwaka 1981.

Mwaka huo, Bayern pia ililazimisha sare ya bila kufungana na Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield na Rummenigge alifunga bao katika mechi ya marudiano iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, lakini Bayern ikaondolewa kwa sheria ya bao la ugenini lililofungwa na Ray Kennedy kwenye uwanja wa Olympic mjini Munich na Liverpool kusonga mbele.

"Tuliondolewa baada ya sare ya bao 1-1 mjini Munich, kwa hiyo hatutakiwi kufanya makosa kama yale ambayo timu yangu ilifanya. Lazima tucheze vizuri katika mechi ya pili," alisema Rummenigge.

Bayern ililinda vizuri lango lake jana na kuichanganya Liverpool, ambayo ndio kwanza imetoka katika mapumziko ya siku kumi, lakini kocha wa Wajerumani hao, Niko Kovac pia alitaka wachezaji wake wamalize kazi jijini Munich.

"Kila mtu alicheza kwa ajili ya mwenzake na unaweza kuona kuwa kama tuna mpangilio kwenye mchezo wetu, ni vigumu kutufunga," alisema Kovac.

"Huo ndio mpango wetu, lakini bado kuna maeneo ya kuboresha.

"Tumefikia lengo letu na kupata sare, sasa hatuna budi kuhakikisha kuwa tunamaliza kazi nyumbani."

Beki wa kati, Mats Hummels alisema mpango wa Bayern kwenye mchezo huo uloilenga kuichanganya safu ya washambuliaji watatu ya Liverpool; Mo Salah, Roberto Firmino na Sadio Mane.

"Ilikuwa ni kuwamaliza nguvu wapinzani na tulifanikiwa," alisema Hummels.

"sasa tuko katika hali ambayo tunaweza kusonga mbele kwa kushiunda nyumbani na hakuna timu inayofurahia kuja Munich." AFP