VIDEO: SADC yawaombea majeruhi, waliopoteza maisha ajali ya moto Morogoro

Muktasari:

Wajumbe wa mkutano wa baraza la mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), wamesimama kwa sekunde kadhaa kuomboleza vifo vya watu 76 vilivyotokea katika ajali ya moto mkoani Morogoro.

Dar es Salaam. Wajumbe wa mkutano wa baraza la mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), wamesimama kwa sekunde kadhaa kuomboleza vifo vya watu 76 vilivyotokea katika ajali ya moto mkoani Morogoro.

Kabla ya kuanza kusoma hotuba yake leo Jumanne Agosti 13, 2019 naibu waziri mkuu wa Namibia na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Netumbo Nandi-Ndaitwah amewataka washiriki wa mkutano huo kutulia kwa sekunde kadhaa.

Ajali hiyo ilitokea Jumamosi Agosti 10, 2019 katika mtaa wa Itingi, Msamvu barabara ya Morogoro-Dar es Salaam baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta.

“Kwa masikitiko makubwa tunaungana na Rais John Magufuli wa Serikali ya Tanzania na wananchi kuomboleza msiba mkubwa baada ya watu kupoteza maisha katika mlipuko wa lori la mafuta, ni majonzi na tunawaombea wapumzike kwa amani,” amesema Netumbo.

Katika mkutano huo, Waziri Netumbo alimkabidhi uenyekiti wa baraza hilo Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi.